TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Juni, 2021 amekutana na kuzungumza na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ili kubadilishana mawazo kuhusu masuala yanayohusu mustakabali wa Taifa.

Mhe. Rais Samia amewahakikishia Waandishi wa Habari kuwa atashirikiana nao kufanya kazi kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi .

Aidha, Mhe. Rais Samia ameziagiza Taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Vyombo vya Habari nchini kwa kuwa Tasnia hiyo ina mchango mkubwa kwa taifa.

Mhe. Rais Samia amesema Vyombo vya Habari vina mchango mkubwa wa kulinda umoja wa kitaifa, Usalama wa nchi na kuchochea shughuli za maendeleo.

Amesema Vyombo vya Habari vinasaidia kufichua maovu kwa jamii, ikiwemo vitendo vya uzembe kazini , rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma.

Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona Mhe. Rais Samia amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiunga na Taasisi za kupambana na ugonjwa huo wa Corona yani Covax Facility.

Pia Serikali imeshapokea zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 470 ambazo nusu ya fedha hizo zitaumika kukabiliana na ugonjwa huo wa corona na nusu nyingine itatumika kusaidia Sekta zilizo athirika na ugonjwa huo.

Amesema Serikali tayari imeyaruhusu Mashirika ya Kimataifa pamoja na Jumuiya za Kimataifa kuingiza chanjo hizo kuchanja raia wao chini ya uratibu wa Wizara ya Afya.

Mhe. Rais Samia ameongeza kuwa Serikali pia imeruhusu Wananchi kuchanja kwa hiyari yao kwani tayari baadhi ya Watanzania hususan wafanyabiashara wameshaanza kuchanja chanjo ya Corona nje ya nchini.

Mara baada ya kuzungumza na Wahariri wa Habari Mhe. Rais Samia amewashukuru kwa kuitikia wito wa  kufika Ikulu Jijini Dar es Salaam na amewatakia kheri katika kutekeleza majukumu yao ya kuelimisha, kuhabarisha umma na Watanzania kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *