TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Agosti, 2021 amehitimisha Ziara yake ya siku mbili nchini Rwanda kwa kutembelea viwanda vitatu na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na viwanda hivyo.

Katika kiwanda cha kwanza cha Inyange kinachotengeneza vinywaji, Mhe. Rais Samia akiwa na mwenyeji wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wamejionea shughuli za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji ya kunywa, maziwa na juisi.

Aidha, Mhe. Rais Samia pia ametembelea kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi cha Mara Phone na kujionea hatua mbalimbali za utengenezaji wa simu kuanzia hatua ya awali hadi kukamilika kwake.

Pia Mhe. Rais Samia ametembelea kiwanda cha uunganishaji magari cha Volkswagen kilichopo nchini humo na kujionea hatua mbalimbali za kuunganisha magari hayo ambayo huuzwa nchini humo.

Mhe. Rais Samia amewaagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe kukutana na wamiliki wa viwanda hivyo ili kutumia fursa zilizopo katika viwanda hivyo ikiwa ni pamoja na kuwauzia malighafi zinazopatikana nchini Tanzania.

Mhe. Rais Samia ameagana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali na kurejea Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza Ziara Rasmi ya siku mbili nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *