TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 06 Agosti, 2021 amezungumza kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kimataifa wa kusaidia Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) Bw. Peter Sands kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Mfuko huo na Tanzania.

Bw. Sands amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika wadhifa wa Urais na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu baina ya mfuko huo na Serikali ya Tanzania.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa katika misaada inayotolewa na Global Fund, Tanzania ni nchi ya tano kutokana na matumizi mazuri ya  misaada hiyo na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu afya hususan kujenga uelewa wa kina kuhusu masuala ya afya.

Kutokana na matumizi hayo mazuri ya misaada, Mkurugenzi huyo Bw. Sands ameahidi  kutoa Dola za Marekani milioni 794 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023.

Bw. Sands pia amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake za kupambana na UVIKO 19, ambapo amesema Bodi ya Mfuko wa Global Fund imeidhinisha Dola za Marekani Milioni 112 kwa ajili ya kusaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Amefafanua kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kununua vifaa vya kuwakinga wahudumu wa afya (PPE), mitungi ya hewa ya Oxygen, kuziongezea uwezo maabara zetu na  kuboresha miundombinu.

Aidha, Bw. Sands amesema Global fund itashirikiana na wataalamu wa Tanzania kutoa elimu kwa wananchi juu ya mabadiliko ya mara kwa mara ya UVIKO 19.

Pia, amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake kwa kuweka mazingira wezeshi ya kupunguza vikwazo vya kikodi vitakavyowezesha Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuweza kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji huyo kwa Mfuko wao kusaidia Tanzania tangu mwaka 2002 katika kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa UKIMWI na matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo, vifaa vya kuwakinga wahudumu wa afya (PPE) pamoja na utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya afya.

Mhe. Rais amemueleza Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa janga  la  UVIKO 19  limekuwa na athari kubwa katika kupambana na magonjwa ya UKIMWI, kifua kikuu na malaria, hivyo inahitajika mikakati madhubuti ya kupambana na magonjwa hayo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewapongeza Global Fund kwa kutimiza miaka 20 ya kuwezesha mifumo ya usimamizi na upatikanaji wa huduma ya afya na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Mfuko huo katika kuimarisha afya za wananchi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *