TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na kuwa tozo za miamala ya simu zimepunguzwa kwa asilimia 30, tozo hizo ni muhimu kwa kuwa zinachangia upatikanaji wa huduma muhimu za jamii.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 02 Septemba, 2021 wakati aliposimama kuwasalimia wananchi wa Tegeta  Jijini Dar es Salaam na Zinga, Bagamoyo mkoani Pwani wakati akielekea Bagamoyo mjini kuendelea kurekodi vivutio mbalimbali vya utalii katika kipindi   maarufu cha Royal Tour.

Amesema Serikali imeamua kuweka tozo hiyo kwa dhamira ya kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali za huduma ambapo katika kipindi cha miezi miwili Serikali kupitia tozo hizo inajenga vituo vya afya 220 pamoja na ukamilishaji wa madarasa 560 katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi hao wa Tegeta (Dar es Salaam) na Zinga (Bagamoyo) kuwa miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano inakamilika kama ilivyokusudiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na miradi mingine mipya.

Akizungumzia ujenzi wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo, Mhe. Rais Samia amesema mradi huo ni mkubwa na Serikali kwa sasa inaupitia upya ili ijiridhishe kwasababu utasaidia kutoa ajira, kukuza uchumi wa pamoja na kuboresha huduma za kijamii.

Kuhusu UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuona umuhimu wa kupata chanjo kwani ugonjwa huo bado upo na unaendelea kupoteza maisha kwa wananchi.

Mhe. Rais amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani kuhakikisha wanamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji katika mkoa huo ili wananchi waendelee na shughuli za maendeleo kwa amani na utulivu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *