TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa fedha za Serikali ili ziweze kutumika vizuri na kuleta tija katika miradi ya kimkakati na kuwaletea wananchi maendeleo.

Mhe. Rais Samia asema hayo tarehe 27 Septemba, 2021 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Uchaguzi wa viongozi wa ALAT uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametaka kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia TEHAMA na kubuni vyanzo vipya vya mapato bila kutumia mabavu katika kukusanya tozo na ushuru.

Pia Mhe. Rais Samia amewaagiza viongozi wa ALAT kuchukua hatua kwa watendaji wote watakaobainika kufanya ubadhirifu ili tija ionekane katika miradi ya maendeleo na kwenye fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameitaka ALAT na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwashirikisha wananchi katika kuandaa miradi ya maendeleo ya kimkakati kwani baadhi ya miradi imeshindwa kufikia malengo kutokana na ushirikishwaji mdogo ama kutoshirikishwa kwa wananchi.

Mhe. Rais Samia ametolea mfano wa baadhi ya miradi kama masoko na stendi kujengwa katika maeneo ambayo wananchi hawafiki na hivyo kutelekezwa au kutumika kwa kusuasua.

Vilevile, Mhe. Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha inapoandaa mipango ya maendeleo inazingatia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ni wa mwisho katika kutekeleza dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata na vijiji kutenga siku maalum kila wiki kusikiliza na kutatua kero za wananchi, zikiwemo za mirathi na migogoro ya ardhi, ambazo zimekithiri nchini.

Pia Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa kwa sasa kipaumbele kikubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga vituo vya afya kwa Tarafa 250, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa barabara pamoja na madarasa.

Kuhusu Ujenzi wa madarasa, Mhe. Rais Samia amesema alilelekeza fedha za Tozo ziende kujenga vituo vya afya na madarasa lakini sasa amepata  fedha mahali ambazo zitajenga  jumla ya  madarasa 15,000 na kuwezesha watoto wote wanaostahili kuanza shule mwezi Januari mwaka 2022 kupata fursa hiyo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Mameya, Wenyeviti, Madiwani na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana na kuacha migogoro kati yao kwasababu tabia hiyo inazorotesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuharibu taswira ya Serikali kwa jamii.

Mhe. Rais amewataka viongozi wa mikoa kuendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki zoezi la kuchanja kwa hiyari ili kujikinga na UVIKO 19, kwa kuwa ugonjwa huo bado ni tishio.   

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *