TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 15 Oktoba, 2021 amefungua barabara ya Sanya Juu – Elerai yenye urefu wa kilomita 32.2 iliyogharimu shilingi bilioni 62.666 ikiwa ni sehemu ya barabara ya kutoka Boma ng’ombe – Sanya Juu  hadi Kamwanga yenye urefu wa kilomita 98.2.

Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali katika kuwatatulia wananchi kero mbalimbali ambapo ujenzi wa kilomita 44 zilizobaki nazo zitajengwa kama ilivyoahidiwa.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kuwa Serikali itazishughulikia changamoto mbalimbali ambazo zinazowakabili.

Mhe. Rais Samia pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro litakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 12.7 litakapokamilika ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 70.

Amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo iweze kuwa na hadhi kamili kama hospitali ya Rufaaa mkoani humo.

Vilevile, Mhe. Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja jipya la Rau lenye urefu wa mita 20 kutoka upande wa Rau hadi upande wa Mamboleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi litakalogharimu shilingi milioni 910.72 ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 65.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amezungumza na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi ambapo amesema pamoja na mambo mengine ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo ni kuja kuona miradi ya maendeleo na kujua changamoto za wananchi wa mkoa huo.

Mhe. Rais Samia amewashukuru wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa na muamko mkubwa wa kuchanja dhidi ya COVID 19 na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Kuhusu ombi la kufufua viwanda mkoani Kilimanjaro, Mhe. Rais Samia amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuona viwanda vingi vinafanyakazi ili viweze kutoa ajira kwa wananchi na kuchangia maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono uamuzi wa Serikali wa ulipaji tozo zitokanazo na matumizi ya mitandao ya simu kwa kuwa zimekuwa na mafanikio makubwa katika kuchangia upatikanaji wa huduma za jamaii kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya nchini, ambapo baadhi ya mataifa ya nje yameanza kuiga utaratibu huo.

Pia, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wanaoishi karibu na Mlima Kilimanjaro kutunza mazingira ili Mlima huo uendelee kuwa na hadhi yake barani Afrika na duniani kwa ujumla  kwani tayari athari za kinadamu zimeanza kuathiri Mlima huo.

Kesho tarehe 16 Oktoba, 2021 Mhe. Rais Samia ataendelea na ziara yake mkoani hapa ambapo atahudhuria Jubilee  ya miaka 50 ya Hospitali ya KCMC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *