TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Longido mkoani Arusha  kuwasimamia watumishi wa Wilaya hiyo ili wawe na maadili na nidhamu na kuwachukulia hatua pale watumishi hao wanaopokosea.

Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo tarehe 18 Oktoba, 2021 wakati akihutubia wananchi wa Longido katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Stendi Mpya ya Longido mkoani Arusha mara baada ya kuzindua mradi wa maji safi na salama uliogharimu shilingi bilioni 15.8.

Amesema ni lazima viongozi wa Wilaya hiyo kusimamia uwajibikaji katika Halmashauri hiyo kwa kulinda makusanyo ya fedha pamoja na kusimamia nidhamu katika maeneo yao.

Mhe. Rais Samia amesema kumekuwa na tabia kwa viongozi Wilayani humo kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wanaokosea katika uwajibikaji kwani kumekuwa na vitendo vya wizi, upotevu wa mapato na uzembe lakini bado viongozi hawawachukui hatua stahiki.

Katika kuhakikisha miundombinu ya mradi wa maji aliouzindua inadumu na kutoa huduma muda wote, Mhe. Rais Samia, amewataka wananachi  na Askari wa Wanyamapori pamoja na Mamlaka zingine kulinda miundombinu hiyo kwasababu Serikali imetumia fedha nyingi katika  mradi huo kwa lengo la kuwapatia huduma ya maji safi na salama.

Akizungumzia  tatizo la baadhi ya vijiji kukosa huduma ya umeme katika Wilaya ya Longido, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa Wilaya hiyo kuwa ifikapo mwezi Desemba mwakani vijiji 133  vilivyobaki vitapata huduma hiyo ya umeme.

Kuhusu tatizo la ajira kwa vijana, Mhe. Rais Samia amesema yeye binafsi na Serikali anaoyoingoza analifanyia kazi suala hilo kwa kujenga mitaa ya viwanda vitakavyosaidia kutoa ajira kwa vijana na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Awali Mhe. Rais Samia emefungua kiwanda cha nyama cha Eliya Food Overseas Ltd kilichopo wilayani humo chenye thamani ya shilingi bilioni 17 na kuahidi kumaliza changamoto ya maji inayoikabili kiwanda hicho ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema kumekuwa na tatizo kwa kiwanda hicho kukosa malighafi ambayo ni mifugo kutokana na kuwepo kwa ushuru mkubwa unaotozwa na Halamshauri ya Longido jambo linalowavunja moyo wafugaji na kuamua kuuza mifugo yao nchini jirani.

Amesema ni vyema suala hilo liangaliwe kwa umakini kwa kuwa mwekezaji wa kiwanda hicho anapata asilimia 30 ya mali ghafi ambayo haitoshelezi mahitaji ya kiwanda hicho yatakayowezesha kupata faida.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi wa Wilaya ya Longido ambao wengi wao ni jamii ya wafugaji kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakapofanyika mwezi Agosti 2022 ili Serikali ijue idadi kamili ya wakazi hao itakayosaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Mhe. Rais Samia amemaliza ziara yake ya siku mbili Jijini Arusha na amerejea Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *