TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Oktoba, 2021 ameshiriki mjadala kwa njia ya mtandao kuhusu kipindi cha mpito wa haki wa tabianchi (A Just Climate Transition) uliondaliwa na Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change), Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika Mkutano huo Mhe. Rais Samia ameungana na Makamu wa Rais wa Nigeria Oluyemi Oluleke Osinbajo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kwa AfrikaDr. Vera Songwe.

Mkutano huo pia uligusia masuala muhimu kuhusu tabianchi pamoja na changamoto zake katika kutekeleza ajenda ya maendeleo barani Afrika.

Katika mjadala huo, Mhe. Rais Samia pamoja na viongozi hao walikubaliana kuwa, upo umuhimu wa kuwa na ushirikiano endelevu kati ya Taasisi za kitaifa na za kimataifa ili kuhamasisha mitaji mbadala, miradi, kanuni, mifumo pamoja na mipango inayotekelezeka. Majadiliano hayo ni muhimu kwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26).

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amepokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Museveni, uliowasilishwa kwake na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Uganda, Dkt. Monica Musenero Masanza Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amemshukuru Mjumbe huyo Maalum Dkt. Monica Musenero Masanza na pia amemuomba amfikishie salamu zake za shukrani kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa kuendeleza ushirikiano mzuri katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *