TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Visiwa vya Comoro kuratibu sekta binafsi pamoja na Serikali ili kutumia fursa za kibiashara zilizopo nchini humo kuhakikisha Tanzania inanufaika na mahitaji ya bidhaa mbalimbali katika nchi hiyo.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 07 Novemba, 2021 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma katika hafla ya kumuapisha Mhe. Pereira Ame Silima kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Visiwa vya Comoro.

Pia, Mhe. Rais Samia amesema mahitaji ya nchi ya Jamhuri ya Visiwa vya Comoro yanaitegemea Tanzania kwa zaidi ya asilimia 80 hivyo kutoa fursa kubwa ya biashara kwa Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemtaka Balozi Pereira kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya biashara, masuala ya kisiasa, na diplomasia kwa kuwa Tanzania na Comoro zina historia ya uhusiano wa muda mrefu.

Hafla ya kumuapisha Balozi Pereira imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Katanga, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vincent Mbogo pamoja na viongozi na watendaji wengine wa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *