TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Novemba, 2021 amekutana na kuzungumza na Mjumbe Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Boris Johnson, kuhusu masuala ya biashara kati ya Uingereza na Tanzania Mhe. Lord Walney.

Mhe. Walney amemueleza Mhe. Rais Samia kuwa jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Uingereza lilofanyika tarehe 16 Novemba, 2021 Jijini Dar es Salaam limekuwa na mafanikio makubwa ambalo litasaidia kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza.

Viongozi hao wamejadili fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja ufanisi katika kuvutia wawekezaji kutoka nchini Uingereza na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao nchini Uingereza.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Bw. Walney kwa kuja nchini na kushiriki jukwaa hilo na kumuhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Uingereza katika kuchochea biashara baina ya nchi mbili hizo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemuomba Mjumbe huyo Maalumu wa Waziri Mkuu wa Uingereza kumfikishia salamu za pongezi kwa Mhe. Boris Johnson kwa mafanikio makubwa ya Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiko ya Tabianchi (COP 26) ambao umetoa matumaini kwa nchi washiriki kuongeza juhudi katika kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Mabenki ya United Bank for Africa (UBA), Dkt. Tony Elumelu kuhusu nyanja mbali mbali za operesheni ya benki hiyo hapa nchini.

Dkt. Elumelu amemhakikishia Mhe. Rais Samia utayari wa benki hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ufadhili wa miradi ya mafuta na gesi.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemueleza Dkt. Elumelu kuwa Serikali ya Awamu ya Sita iko tayari kufanya kazi na benki hiyo hivyo kumkaribisha kuwekeza kwenye miradi husika.

Vilevile, Mhe. Rais Samia pia amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya DP World toka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sultan Ahmed Bin Sulayem ambapo katika mazungumzo hayo wameonyesha nia ya kuimarisha  ufanyaji biashara nchini Tanzania katika maeneo ya bandari, uchukuzi, kongani za viwanda  na sekta ya nishati.

Pia, Mhe. Rais Samia amezungumza kwa njia ya mtandao na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Equinor inayowekeza katika mafuta na gesi, Bw. Anders Opedal.

Bw. Opedal amemuhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa kampuni kwa kushirikiana na kampuni ya Shell wapo tayari kuendelea na majadiliano na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa gesi hapa nchini. 

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameeleza utayari wa Serikali kuona majadiliano kuhusu mradi wa gesi yanafanyika kwa manufaa ya pande zote mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *