TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wanawake wa Tanzania kwa kuchangia kwa hali na mali katika kuleta maendeleo nchini Tanzania.

Mhe. Rais Samia ametoa pongezi hizo tarehe 20 Novemba, 2021 wakati akihutubia katika Mkutano wa kumpongeza kwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi vinara duniani katika masuala ya haki, usawa wa kijinsia na kiuchumi, ulioandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Amesema maendeleo yanayoonekana nchini yanatokana pia na amani na utulivu inayochangiwa na kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeonyesha matumaini makubwa katika kuleta na kudumisha amani na utulivu wa Zanzibar.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Wazanzibari kuendelea kudumisha amani iliyopo kwa kuilinda na kuiendeleza misingi imara iliyopo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kudumisha amani iliyopo na kuyaenzi malengo ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo miongoni mwao ni amani, umoja na mshikamano.

Aidha, Mhe. Rais amewataka wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022 ili kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kutekeleza vizuri mipango ya maendendeleo.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza muda wa mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kuiongoza Zanzibar na kuendelea kuiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Pia, Mhe. Rais Samia amewakumbusha na kuwaomba Wanawake wa Umoja wa Wazazi Tanzania (UWT) kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mwaka 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *