TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 23 Novemba, 2021 amezindua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa iliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Mhe. Rais Samia amesema jukumu la usalama barabarani sio la Askari wa barabarani peke yao bali  ni la kila mwananchi  katika jamii na hivyo kumtaka kila mwananchi kuwa makini na kuhakikisha matumizi sahihi ya barabara.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema suala la usalama barabarani lipewe uzito wa kuwa ajenda ya kitaifa katika majukwaa pamoja na kuwahusisha kikamilifu washirika wa maendeleo hasa wale ambao wamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya nyanja ya usalama barabarani.

Mhe. Rais Samia amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa ajali za barabarani bado zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania wengi mbali na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu bora ya barabara.

Vilevile, Mhe. Rais amesema vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani ambapo asilimia kubwa za ajali hizo husababishwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.

Mhe. Rais Samia amesema takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano jumla ya wapanda pikipiki 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kusababisha majeruhi 4,202.

Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuwa na msaada kwa wananchi na sio kero kwao ili kujenga mahusiano mazuri katika jamii hali itakayopelekea kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali kwa wakati.

Ametaja baadhi ya kero zinazofanywa na Askari wa usalama barabarani kuwa ni pamoja na kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu, kulazimisha madereva kulipa faini za papo kwa papo kinyume na ilivyo Sheria ya Usalama Barabarani, hivyo kuwataka wahusika kubalika mara moja.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikianana na vyuo vikuu, vyuo vya ufundi  na chuo cha Usafirishaji (NIT) kuwekeza katika utafiti wa suala la usalama barabarani ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabarani.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amelitaka Baraza la Usalama Barabarani kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu ya usalama barabarani kwasababu kwa hivi sasa dunia ni ya kidijitali na taarifa nyingi zipo kiganjani ambapo vijana wengi hutumia mitandao hiyo.

Pia, Mhe. Rais Samia ameelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa magari kabla ya kutoa stika za usalama barabarani na kutaka Taasisi zinazohusika kukaa na wadau na Sekta binafsi kujadiliana jinsi ya kuendesha zoezi hilo kwa pamoja kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Katika Maadhimisho hayo ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Mhe. Rais Samia amekabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani vilivyotolewa na wadau mbalimbali. Pia, Mhe. Rais alitembelea mabanda mbalimbali pamoja na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na wadau mbalimbali kuhusu usalama barabarani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *