TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi Bi. Patricia Danzi leo tarehe 26 Novemba, 2021 Jijini Dodoma.

Katika Mazungumzo hayo, Bi. Danzi amempongeza Mhe. Rais Samia kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini Tanzania kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani ikiwa ni pamoja na Serikali kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kurudi shuleni.

Bi. Danzi amemueleza Mhe. Rais Samia kuwa Serikali ya Uswisi imekuwa na ushirikiano wa kimaendeleo na Serikali ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 40  katika sekta za afya, elimu katika masuala ya utafiti na kuwawezesha vijana katika mipango mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Mhe. Rais Samia pia amemueleza Bi. Danzi hatua zinazo chukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu,  maji, afya na nyinginezo.

Kuhusu UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amemueleza Bi. Danzi kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabilaiana na ugonjwa huo ikiwemo kutoa chanjo na elimu kwa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Mhe. Rais Samia amewasili Jijini Dar es Salaam leo akitokea Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *