TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kufuatia ubadhirifu unaofanywa katika Taasisi zao na kuisababishia hasara Serikali.  

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 04 Desemba, 2021 katika hafla ya uzinduzi rasmi wa matumizi ya Mradi wa Maboresho ya Miundombinu ya Gati namba 0 hadi 7 pamoja na uongezaji wa kina cha bahari katika lango kuu la bandari katika hafla iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema pamoja na makusanyo yanayofanywa na TPA, bado zipo changamoto za upotevu wa mapato unaochangiwa na kutokuwepo  kwa mfumo madhubuti, na hivyo kuwepo kwa mianya mingi ya upotevu wa mapato.

Mhe. Rais Samia amesema Taarifa ya Ukaguzi Maalum wa Kiuchunguzi wa Mfumo wa Enterprise Resource Planning (ERP) katika Mamlaka hiyo ya Bandari uliofanyika kuanzia Juni, 2020 na Ripoti yake kutolewa Machi, 2021 imeonesha upotevu wa fedha nyingi zilizotumika kuajiri Makampuni mbalimbali ya kuanzisha mifumo ya kielekroniki ya ukusanyaji wa mapato ambayo haikutoa tija iliyokusudiwa.

Aidha, Mhe. Rais Samia amezitaja Kampuni hizo kuwa ni Soft Tech Consultant Ltd ambayo ilipewa zabuni ya shilingi milioni 694  na kulipwa shilingi milioni 600, Kampuni ya Twenty Third Centuary System ilipewa kazi ya Dola za Marekani milioni 6.6 na kulipwa Dola milioni 4.6 na mkataba kuvunjwa na Kampuni ya  SAP – East Africa Ltd iliyopewa Dola za Marekani 433,000 Mshauri Mwelekezi binafsi alilipwa Dola za Marekani 31,920.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema anazo taarifa kwamba kupitia mifumo hiyo mibovu, Watumishi wa kitengo cha Hesabu wanashirikiana kuchezea mifumo na kudanganya kwamba mizigo imelipiwa na mifumo magetini kusoma malipo yamefanyika na kuruhusu kutoka ilhali mizigo hiyo ikiwa haijalipiwa.

Kufuatia ubadhirifu huo, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kupitia ripoti hiyo na kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika.

Mhe. Rais Samia pia amezungumzia ubadhirifu katika mradi wa ujenzi wa Meli tano za Kampuni ya huduma za Meli (MSCL) zinazojengwa na kuwataka wahusika kuchukua hatua haraka .

Katika hatua nyingine Mhe. Rais Samia ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi  yaendayo Haraka awamu ya pili (BRT II) katika Barabara ya Kilwa-Chango’mbe na Kawawa yenye urefu wa kilomita 20.3. 

Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia amesema kukamilikika kwa ujenzi wa Mradi huo kutasaidia kupunguza msongamano na ajali za barabarani na kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa ukanda huo wa kuelekea mikoa ya Kusini mwa nchi yetu.

Mhe. Rais Samia amesema mbali na ujenzi wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka (BRT), Serikali inaendelea na jitihada za kufanya maboresho mbalimbali kama vile upanuzi wa barabara na ujenzi wa barabara za juu (flyovers) ili kukabiliana na kero ya msongamano wa magari.

Pia Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa tayari Serikali imepata mkopo kutoka Benki ya Dunia utakaowezesha kuendelea na ujenzi wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto.

Aidha, Mhe. Rais Samia amekemea vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu na kuwataka wananchi kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo hivyo ambavyo ni sawa na uhujumu na vinachelewesha ukamilishaji wa miradi hiyo.

Mhe. Rais Samia amesema wapo baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo ya ujenzi ya hifadhi ya barabara na kujenga vibanda vya biashara bila kujali maelekezo yanayotolewa hivyo kuhatarisha usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Pia, amesema kuna vitendo vinafanywa na baadhi ya watumiaji wa barabara kama vile kuzidisha uzito wa magari, kumwaga mafuta barabarani, kuziba mifereji ya maji, uegeshaji holela wa magari ambavyo vinachangia kuharibu mazingira kwa ujumla.

Kufuatia vitendo hivyo, Mhe. Rais Samia ameagiza kufanyika kwa doria za mara kwa mara katika maeneo hayo na hatua kali zichukuliwe kwa wote wanaokiuka maelekezo hayo.

Mhe. Rais amewaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO 19 katika wimbi la nne ambalo tayari limezikumba nchi kadhaa Barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *