TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 14 Januari, 2022 amepokea Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Évariste Ndayishimiye uliowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye ni Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi Mhe. Ezechiel Nibigira, Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.

Mhe. Nibigira amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kukubali kupokea Ujumbe huo Maalum na kufikisha salamu kutoka kwa Mhe. Rais Ndayishimiye na kumjulisha kuwa hali ya Burundi ni salama na tulivu, hivyo kupelekea wananchi wake kuendelea na shuguli mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Amesema Mhe. Rais Ndayishimiye amemtuma kufikisha ujumbe huo wenye lengo la kukuza zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Burundi katika masuala ya kiuchumi.

Aidha, Mjumbe huyo Maalumu Mhe. Nibigira amesema Tanzania na Burundi imekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika masuala ya diplomasia na siasa na kwa sasa nchi hiyo imeamua kushirikiana katika mambo ya kiuchumi yatakayonufaisha nchi zote.

Ameongeza kuwa ipo miradi mbalimbali inayotarajiwa kutekelezwa na nchi hizi mbili ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) utakaounganisha Tanzania na Burundi.

Mhe. Nibigira amesema kukamilika kwa Ujenzi wa reli hiyo kutasaidia usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo madini ya Nickel ambayo yanapatikana nchini Burundi na Tanzania na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi katika nchi zote mbili.

Aidha, Mhe. Nibigira amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano ambao Burundi inaupata kutoka Tanzania katika masuala mbalimbali.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amepongeza Mhe. Rais Ndayishimiye kwa jinsi anavyoendesha nchi na kuendeleza amani ambayo inawezesha wananchi wa nchi hiyo kupiga hatua kimaendeleo.

Pia, Mhe. Rais Samia amemhakikishia Mhe. Rais Ndayishimiye kuwa Tanzania itaendelea kuungana na Burundi katika masuala mbalimbali ya uhusiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kuhusu suala la Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha Tanzania na Burundi, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania imekwisha anza ujenzi wa reli hiyo na kuhusu kipande cha kuunganisha nchi hizo hatua mbalimbali zinaendelea.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amepokea Hati za Utambulisho wa Mabalozi wanne walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.

Mabalozi waliowasilisha Hati za Utambulisho ni: –

  1. Mhe. Abdulla Ali M. Alsheryan – Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini;
  2. Mhe. Kim Sun Pyo – Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini;
  3. Mhe. Triyogo Jatmiko – Balozi wa Indonesia hapa nchini;
  4. Mhe. Zakaria El Goumiri – Balozi wa Morocco hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kupokea hati hizo, Mhe. Rais Samia amewapongeza Mabalozi hao na kuwaomba kufikisha salamu zake kwa Viongozi Wakuu wa nchi zao na kusisitiza kuwa Tanzania itazidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.

Kwa upande wao, Mabalozi hao wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa utendaji mzuri wa kazi na kumuahidi ushirikiano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *