RAIS SAMIA AMEKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA SHEIKH MOHAMMED BIN RASHID AL MAKTOUM
Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyeko ziarani Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amekutana na kufanya mazungumzo na Sheikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Falme hizo .
Rais Samia na Sheikh Maktoum ambaye pia ni Mtawala wa Dubai wameshuhudia uwekwaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) katika ushirikiano kwenye diplomasia.
Tanzania itanufaika zaidi kwa kuzingatia hatua kubwa iliyopigwa na UAE kiuchumi ambapo itatumia fursa hiyo kuchagiza zaidi utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amezihakikishia Falme hizo za Kiarabu kuendeleza ushirikiano uliodumu kihistoria miaka mingi baina yao na Tanzania.
“Naahidi ushirikiano wa kijamii na kiuchumi pamoja na kisiasa kuimarishwa na kuendelezwa kwa manufaa ya watu wetu”.
Rais Samia aliyasema hayo akihutubia katika Siku ya Kitaifa ya Tanzania kwenye maonesho ya Dubai Expo 2020, tukio ambalo lilitoa fursa pia ya Tanzania kuonyesha vivutio vyake mbalimbali kwa raia wa takriban nchi 192. Baadhi ya vivutio vikuu ni mbuga za wanyama, madini na fursa za uwekezaji katika nyanja mbalimbali.
Waziri wa Ustahamilivu na Utengamano ambaye pia ni Kamishna wa Expo 2020, Sheikh Nahayan Mabarak Al Nahayan, amesema UAE iko tayari kutumia kila fursa kuimaraisha uhusiano wa pande zote mbili.
‘Kwa mantiki hiyo tunakusudia kukuza ushirikiano wetu na Tanzania kwa masuala mbalimbali yanayofanana kama vile huduma za afya, miundombinu, na kuunga mkono wajasiriamali wadogo na wa kati”.
Dubai ni jiji la kwanza Mashariki ya Kati kuandaa maonesho makubwa ya kimataifa yajulikanayo kama World Expo tangu yalipoanzishwa mwaka 1851.