TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI WA SAINI WA HATI YA USHIRIKIANO NCHINI UGANDA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Ushirikano (MoU) mbili Ikulu Entebbe nchini Uganda.

Hati hizo ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400KV kutoka Masaka-Mutukula-Nyakanazi -Mwanza na nyingine ni kuhusu ushirikiano wa masuala ya Ulinzi na Usalama baina ya nchi hizo mbili.

Aidha, utiaji saini huo ulishuhudiwa pia na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambapo amesisitiza kuendelea kushirikiana kwenye utenngenezaji wa chanjo na dawa za binadamu na mifugo.

Makubaliano pia ni kwamba Tanzania itaanza kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) kutoka Uganda.

Miongoni mwa mengine yaliojadiliwa ni kufunguliwa upya kwa njia ya Mwanza – Port Bell Kampala, ambayo hapo awali ilikuwa haifanyi kazi lakini hivi sasa inafanya kazi.

Kwa sasa njia hiyo imepunguza kwa kiwango kikubwa muda wake wa mpito ambapo sasa huchukua siku 4 tu tofauti na siku 9 hapo awali, hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara.

Wakati huo huo, Tanzania imekubali kupunguza gharama za usafirishaji ambapo kwa sasa Uganda italipa Dola za Kimarekani 10 kwa lori litakalopita kila kilomita 100 katika njia ya kutoka Mutukula hadi Dar es Salaam kuanzia mwaka mpya wa fedha Julai mosi mwaka huu.

Pia, Uganda imeahidi kutuma tani nyingine elfu 10 za sukari ili kufidia upungufu wa bidhaa hiyo Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *