RAIS JAKAYA KIKWETE AZINDUA MRADI WA MAJI MASASI – NACHINGWEA (MANAWASA).

ANGALIA VIDEOJINSI RAIS DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE ALIVYOFUNGUA MRADI WA MAJI WA NACHINGWEA MASASI (MANAWASA) https://www.youtube.com/watch?v=xClj3nmoXU8 KERO YA KARNE YA MAJI YAMALIZIKA MASASI NA NACHINGWEA Kero ya miaka mingi ya uhaba mkubwa wa maji kwa wakazi wa miji ya Masasi, Mkoa wa Mtwara na Nachingwea,  Mkoa wa Lindi, hatimaye imemalizika kufuatia kuzinduliwa kwa mradi mkubwa ambao unatoa huduma ya maji kwa wakazi wa miji hiyo.       Aidha, mradi huo, unaojulikana kama Mradi wa Majisafi wa Masasi –Nachingwea, utatoa maji pia kwa baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi pia, na vijiji vingine ambako mradi huo unapitia. Mradi huo mkubwa wenye uwezo wa kutoa lita za ujazo za maji milioni 13.6 kwa siku kutoka chanzo cha maji cha chemichemi ya Mbwinji iliyoko Milima ya Makonde katika Wilaya ya Newala, umezinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Julai 24, 2014, katika sherehe kubwa zilizofanyika katika miji hiyo miwili ya Masasi na Nachingwea.  Mradi huo ulioanza kujengwa Februari 2011 na kukamilika Julai mwaka jana, umejengwa chini ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa gharama kubwa ya kiasi cha sh. bilioni 31 na unaendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA). Gharama za mradi huyo zimetolewa kwa pamoja na Serikakli ya Tanzania na mfuko wa wafadhili ambao wanahisa sekta ya maji ikiwamo Benki ya Dunia na wafadhili wengine wengi. Kwa mujibu wa maelezo ya Mhandisi Nuntufyo David Mwamsojo, mbali na mradi huo kuwa na uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 13.6, mahitaji ya mji wa Masasi kwa sasa ni mita za ujazo milioni mbili tu na yale ya Nachingwea ni milioni 1.25 kwa hiyo kuuacha mradi huo kubakia na uwezo mkubwa wa kuhudumia miji hiyo kwa miaka mingi ijayo. Alisema kuwa huduma ya maji, kufuatia kukamilika kwa mradi huo, inawafikia wakazi 83,128 kati ya wakazi 102,696 sawa na asilimia 81 ya wakazi wote wa mji wa Masasi wakati kwa mji wa Nachingwea mradi unatoa huduma kwa wakazi 49,471 kati ya wakazi 77, 207 ambayo ni sawa na asilimia 64. Mpaka sasa wateja 2,101 wameunganishiwa maji kutoka mradi huo katika mji wa Masasi wakiwemo wateja 1,721 wapya wakati katika mji wa Nachingwea wateja zaidi ya 900 wameunganishiwa  huduma ya maji ya mradi huo mpya wakiwemo 371 wapya. Kukamilika kwa mradi huo kunatimiza ahadi ambayo Rais Kikwete aliitoa wakati wa Kampeni ya uchaguzi Mkuu na hivyo kuwawezesha wakazi wa maeneo hayo kuboresha maisha yao kwa kuwa na maji safi na salama. Akizungumza katika sherehe zote mbili za Masasi, wakati wa asubuhi na Nachingwea, wakati wa mchana, Rais Kikwete ametoa maombi mawili kwa wakati wa mji huo. Kwanza, amewataka wakazi wa maeneo hayo kulinda chanzo cha maji hayo katika Milima ya Makonde katika Wilaya ya Newala, na pili ni kulinda miundombinu ya kusambaza maji hayo popote ilipo. “Mimi kama mnavyojua, niliishi Nachingwe kati ya mwaka 1986 na 1988 kabla ya kuhamishiwa Masasi, hivyo mimi siyo mgeni kwa tatizo kubwa la maji lililokuwa linawakabili wananchi. Nalielewa vizuri. Nimeishi nalo. Hivyo, ninaposema nafurahi kwamba tumemaliza tatizo hilo, maneno hayo yanatoka ndani ya dhati ya moyo wangu,” amesema Rais Kikwete. Rais Kikwete, wakati huo akiwa Meja Kikwete, alikuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nachingwea kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Masasi na hatimaye kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini mwaka 1989.             Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma na siku moja moja katika mikoa ya Lindi na Mtwara amerejea Dar Es salaam jioni ya leo. bahati Mohamed

 

machine Fundi mitambo Shida Mohamed akitoa maelezo kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete jinsi mashine za kusukuma maji kutoka kwenye chanzo cha maji kwenda kwenye tank la kuhifadhi majizinavyofanya kaziP1020977 Mashine za kusukuma maji kutoka kwenye chanzo cha maji kwenda kwenye tank 3 (2) Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akibonyeza kitufe kuashiria ufunguzi wa mradi mkubwa wa maji Nachingwea Masasi (MANAWASA)  P1020983 Tank kubwa la kuhifadhi maji    

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *