TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AHIMIZA WANANCHI KUWEKEZA KATIKA KILIMO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameuagiza kila mkoa kutenga eneo litakalotumika kwa kilimo cha mazao yanayozalishwa katika mkoa husika.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima (Nanenane) iliyofanyika katika uwanja wa John Mwakangale.

Aidha, Rais Samia amewataka wakulima kutumia maeneo hayo yatakayotengwa kuzalisha kibiashara ili kupata chakula cha kutosha na kuuza kwa nchi jirani.

Vile vile, Rais Samia amewataka wakulima kujisajili ili kupata vitambulisho ambavyo vitatumika kupata ruzuku ya mbolea kuendana na misimu.

Rais Samia pia amemuelekeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Chuo cha Kilimo (SUA) ili kuwezesha vijana wanaohitimu chuoni hapo kuweza kujiajiri katika sekta hiyo.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameitaka Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa NARCO kufanya uchambuzi wa vitalu vya ranchi vilivyokodishwa na kujua mapato yatokanayo na vitalu hivyo.

Halikadhalika, Rais Samia ameiagiza Wizari ya Mifugo na Uvuvi kufuta leseni za vitalu vilivyokodishwa na kupanga upya ili kufanya uwekezaji wenye tija.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AFANYA ZIARA YA KIKAZI WILAYA RUNGWE NA KYELA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema mkoa wa Mbeya unakabiliwa na changamoto ya lishe bora kwa watoto licha ya kuwa mkoa huo unalima na kuzalisha chakula kwa wingi.

Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa John Mwakangale wilayani Kyela.

Aidha, Rais Samia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha anatekeleza Mpango wa Pili Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (NMNAP II 2021 – 2026).

Vile vile, Rais Samia amewataka wananchi wa mkoa huo kuongeza jitihada katika masuala ya lishe bora ili kuimarisha afya za watoto.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuwa na umoja na mshikamano na kufanya kazi kwa kushirikiana bila ya kujali itikadi zao. Rais Samia ameendelea na ziara yake mkoani Mbeya ambapo leo ametembelea Wilaya ya Rungwe na Kyela na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha mpakani mwa Tanzania na Malawi