Category Archives: Uncategorized

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AWATAKA MAWAKILI WA SERIKALI KUTOA ELIMU KWA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya Sheria za uwekezaji pamoja na biashara nchini ili kukabiliana na migogoro inayotokana na Sheria hizo.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Aidha, Rais Samia amesema ni vyema Mawakili wa Serikali wawe makini na kuharakisha kusikiliza migogoro inayokinzana na Sheria za uwekezaji ili kupunguza kupelekana Mahakamani na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Rais Samia amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kesi za uwekezaji, kulinda uwekezaji nchini na kupanua wigo wa kukuza uwekezaji, kukusanya mapato na hivyo kukuza uchumi kwa maslahi ya taifa.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kukiuka haki za wananchi na kuwasaidia kutatua kero zao ambazo hazihitaji kufikishwa mahakamani.

Rais Samia pia ametoa wito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Mawakili wote wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan sheria zinazowagusa wananchi na kuwaelekeza taratibu za namna ya kupata haki zao.

Vile vile, Rais Samia amesema utoaji wa elimu utapunguza mrundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya utatuzi na hivyo pia kuchangia kupunguza mrundikano wa mahabusu. Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa kutumia Kamati za Ushauri wa Kisheria zilizoanzishwa katika ngazi zote za Mikoa na Wilaya nchini kupunguza malalamiko ya wananchi na mashauri dhidi ya Serikali.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aweka Shada la Maua katika eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa nchi ya Msumbiji (Mozambican Heroes’ Square) tarehe 21 Septemba, 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitembelea na kuweka shada la Maua katika eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa nchi ya Msumbiji (Mozambican Heroes’ Square) lililopo Maputo nchini humo tarehe 21 Septemba, 2022. Mhe. Rais Samia aliweka Shada hilo kwa Heshima ya kuwakumbuka Mashujaa wa Msumbiji akiwemo Rais wa Kwanza wa Nchi hiyo Hayati Samora Machel
.
Viongozi mbalimbali kutoka Tanzania wakiwa katika eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa nchi ya Msumbiji (Mozambican Heroes’ Square) lililopo Maputo nchini humo tarehe 21 Septemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia vikundi vya ngoma za asili za Msumbiji wakati akitoka kuweka shada la maua kwenye eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa nchi hiyo (Mozambican Heroes’ Square) lililopo Maputo tarehe 21 Septemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mji wa Maputo mara baada ya kutembelea Kituo cha uzalishaji wa Nishati ya Umeme nchini Msumbiji tarehe 21 Septemba, 2022.