Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha anaimarisha chama cha Skauti nchini kutokana na kazi yake nzuri katika jamii ikiwemo kuunganisha vijana bila kujali dini, kabila, rangi, jinsia au itikadi ya kisiasa.
Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 02 Oktoba, 2021 wakati akizungumza katika siku ya Mlezi wa Skauti nchini iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Aidha, Mhe. Rais Samia amekitaka Chama cha Skauti nchini, Girl Guides, na umoja wa vijana wa vyama vya siasa kuangalia suala la maadili kwa vijana na kutathmini mwenendo wao kwa kuwa licha ya kuwepo kwa mfumo mkubwa wa Taasisi hizo katika shughuli zake bado kumeendelea kuwepo na mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema Chama cha Skauti kimesaidia kuitangaza nchi katika mikutano mbalimbali ambayo wamekuwa wakishiriki au kuindaa, mathalami Mkutano wa Skauti Kanda ya Afrika wa mwaka 2017 ambapo Chama cha Skauti Tanzania ilikuwa mwenyeji.
Mhe. Rais Samia amesema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Chama cha Skauti nchini na mafanikio yaliyopatikana, Chama hicho bado kinakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na idadi ndogo ya wanachama na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amewataka Viongozi na Wanachama wa Skauti kujikinga na kuwahamasisha wananchi wengine kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO 19, ikiwemo kupata chanjo na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Agosti 2022.
Mhe. Rais Samia amewataka Skauti nchini kushiriki kikamilifu katika kutangaza mafanikio yaliyopatikana nchini katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 59 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Ulimwengu uweze kuyafahamu.
Katika hafla hiyo, Kamishna wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Salum Hamduni, amemkabidhi Mhe. Rais Samia Miongozo ya kuwawezesha na kuwafundisha vijana wa Skauti jinsi ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Pia, Mhe. Rais Samia amewavisha Nishani Viongozi na watu mbalimbali waliochangia katika kuleta mafanikio ya Chama cha Skauti nchini.