Daily Archives: October 18, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu kumaliza ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo kwa kuwa hakuna sababu ya ujenzi huo kutokukamilika wakati Serikali tayari imeshapeleka fedha za ujenzi wa hospitali hiyo.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 17 Oktoba, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

Mhe. Rais Samia amesema lengo la ziara yake mkoani Arusha ni kukagua miradi ya maendeleo na kuwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kazi kubwa waliyofanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Arusha kuwa tatizo la maji katika mkoa huo litakuwa historia ifikapo mwezi Juni 2022 mradi huo utakapokamilika na kuwapatia huduma ya maji safi na salama wananchi wote.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, imepeleka shilingi bilioni 90.2 mkoani humo katika kusaidia sekta ya utalii ambayo imeathirika na janga hilo ambapo pia Serikali inaimarisha sekta hiyo kwa kuwakaribisha wawekezaji ambao watawekeza katika ujenzi wa hoteli za nyota tano nchini.

Akizungumzia suala la viwanda ambavyo havifanyi kazi mkoani humo, Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali imeandaa mpango wa kuweka kongano la viwanda ambalo litafungua uwekezaji wa viwanda takriban 20 na kutoa ajira kwa vijana wa mkoa huo.

Kuhusu suala la vijana kukosa ajira, Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali iko katika mazungumzo na wawekezaji ambao wanakusudia kujenga kiwanda cha TEHAMA ambacho kitasaidia vijana wengi kupata ajira kupitia sekta hiyo.

Aidha, Mhe. Rais amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kukutana na viongozi wa kabila la kimasai ili wamalize mgogoro uliopo katika hifadhi ya Ngorongoro.

Mapema asubuhi, Mhe. Rais Samia amekagua ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji  na usafi wa mazingira unaogharimu shilingi bilioni 520, katika eneo la Chekereni mkoani Arusha.

Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Arusha, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama  katika mkoa wote ambapo ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 75.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amefungua Majengo mapya ya Hospitali ya Jiji la Arusha yaliyojengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halamashauri ya Jiji hilo pamoja na kutembelea mabanda ya wajasiriamali wadogo wa mkoa huo.

Mhe. Rais Samia amekabidhi hundi zenye jumla ya shilingi Bilioni 1.39 kwa vikundi vya wanawake, walemavu na vijana ikiwa ni mkopo kutoka fedha zinatokana na makato ya asilimia 10 ya Hamashauri ya Jiji la Arusha.

Mhe. Rais Samia ameagiza Halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuwezesha makundi yenye uhitaji kupata mikopo ambayo itawasaidia kujikwamua na umasikini.

Kesho tarehe 18 Oktoba, 2021 Mhe. Rais Samia ataendelea na ziara yake mkoani humo ambapo atatembelea Wilaya ya Longido na kuzindua mradi wa maji na kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya Food Overseas Limited pamoja na kuzungumza na wananchi.

Siku ya Kwanza ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Arusha Tarehe 17 Oktoba, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuzindua rasmi Hospitali ya Jiji la Arusha katika Eneo la Njiro Jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimsalimia mtoto Nassir Mbarouk  aliyezaliwa usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Jiji la Arusha muda mfupi baada ya kuziindua rasmi Hospitali hiyo iliopo katika eneo la Njiro Jijiini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimsalimia mtoto Samia Yona  aliyezaliwa usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Jiji la Arusha muda mfupi baada ya kuziindua rasmi Hospitali hiyo iliopo katika eneo la Njiro Jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wananchi wa Chekereni Arumeru Mkoani Arusha mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa Maji safi na Salama unaoendelea katika eneo hilo.
.
.
.
.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi Hundi ya shilingi milioni 387,380,675.00 kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu katika Tarafa ya Themi Mkoani Arusha .
.
Viongozi wa dini wakimsikiliza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha
Wananchi wakimsikiliza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha
Viongozi na wananchi wakimsikiliza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha
.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Wananchi wa Arusha  mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na  Wananchi wa Arusha mara baada ya kuhutubia mkutano wa Hadhara katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
.
.