Daily Archives: October 24, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 23 Oktoba, 2021 amehudhuria kilele cha maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kumbukumbu ya Bibi Titi Mohamed, katika sherehe zilizofanyika kwenye kijiji cha Mkongo Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Samia amesema ipo haja kwa viongozi wa UWT kujitathimini katika kipindi cha miaka 60 tangu nchi ipate uhuru kuangalia kama wanaendeleza yale yaliofanywa na waasisi wa Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na Bibi Titi Mohamed.

Mhe. Rais Samia amesema katika kipindi hiki ambacho nchi inatimiza miaka 60 ya uhuru ni vyema viongozi wa Umoja huo wakajiridhisha namna ulivyoweza kumkomboa mwanamke wa Tanzania.

Amesema wakati wakitathmini mchango wa muasisi wa Umoja huo Bibi Titi Mohamed, wanapaswa kuangalia namna safari ya UWT ilivyokuwa kwa kutazama hali ya kiuchumi, kisiasa na kifikra pamoja na walivyoweza kumkomboa mwanamke.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema ameupongeza UWT kwa kutayarisha viongozi ambao wamesaidia kubadili mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kuweza kuwa na viongozi wanawake walioshika nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

Mhe. Rais Samia amesema kutokana na hali hiyo hivi sasa wanawake nchini wanapaswa kuungana pamoja ili kutimiza malengo ya Serikali na kuwezesha jamii kupata maendeleo.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali inatambua mchango wa Bibi Titi alioutoa kwa taifa ambao ulisababisha  Serikali kuipa jina lake katika moja ya barabara ya Jiji la Dar es Salaam kama ishara ya kumuenzi na kutambua mchango wake.

Amesema Bibi Titi wakati wa uhai wake alitumia sauti yake kudai maslahi ya wanawake katika nyanja mbalimbali pamoja na kupaza sauti katika Jumuiya za Kimataifa na kuwezesha hivi sasa wanawake wa Tanzania kusikilizwa.

Mhe. Rais Samia amewataka watafiti na waandishi katika fani za historia kuandika vyema historia ya Bibi Titi Mohamed ili kuwezesha vizazi vya sasa na vijavyo kujua kikamilifu mchango wake kwa taifa.

Kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa wa Pwani, Mhe. Rais Samia amesema kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, mkoa huo ni wa pili kwa kupata fedha nyingi ambazo zitatumika katika ujenzi wa madarasa kwenye shule shikizi pamoja na shule zenye mahitaji maalum.

Amesema fedha hizo pia zitatumika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya afya katika Halmashauri za Kibaha, Mafia pamoja na ununuzi wa mashine za X – Ray  kwa ajili ya wilaya za Kibiti na Chalinze.

Mhe. Rais Samia amupongeza Umoja wa Wanawake Tanzania kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanza kujenga majengo ya Makao Makuu yake Jijini Dodoma, vibanda vya biashara 302 pamoja na mashine za kukobolea nafaka.