Daily Archives: October 25, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 25 Oktoba, 2021 amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) Bi. Preeti Sinha, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Bi Sinha amemueleza Mhe. Rais Samia kuwa UNCDF ipo tayari kushirikiana na nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Serikali ya Tanzania kutafuta njia mbadala za kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Bi Sinha amesema kupitia Mradi wao ujulikanao kama Municipal Investment Financing, unaweza kusaidia upatikanaji wa fedha kwa Serikali za Mitaa kupitia uanzishwaji wa Hati Fungani

Fedha zitakazo patikana kupitia Hati Fungani zitarejeshwa kutokana na makusanyo yanayopatikana kwenye Serikali za Mitaa

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amekubaliana na wazo hilo na kusema kuwa litasaidia kupunguza mzigo kwa Serikali Kuu kuhudumia miradi ya maendeleo ya Serikali za Mitaa.

Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uratibu utakaowezesha mpango huo kuanza kutekelezwa mara moja.