Daily Archives: May 25, 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA APOKEA TUZO YA MJENZI MAHIRI YA BABACAR NDIAYE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea tuzo ya Babacar Ndiaye (2022) kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

Tuzo hiyo alipokea katika Mkutano wa 57 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo hupewa viongozi wa Afrika walio mstari wa mbele katika kuendeleza miundombinu.

Katika hafla hiyo, Rais Samia ametoa wito kwa nchi za Afrika kuungana, kuzijenga na kuziwezesha jumuiya za kiuchumi za kikanda na bara zima kwa ujumla.

Rais amesema lengo la ujenzi wa miundombinu Tanzania ni kuunganisha nchi, ukanda wa Afrika Mashariki na nchi za SADC ili kufikia agenda ya utangamano wa Afrika kiuchumi na kijamii.

Wakati huo huo, Rais Samia amesema ni lazima Afrika izalishe, ichakate na ifanye biashara ndani ya bara ili Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) liweze kutimiza malengo.

Vile vile, Rais Samia amesema maendeleo ya miundombinu ni mchakato endelevu, hivyo anatambua michango ya Marais waliotangulia katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini kupitia Mfuko wa Barabara na Taasisi za kifedha za kimataifa.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UTEUZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Viongozi kama ifuatavyo:-

  1. Amemteua Bi. Sauda Kassim Msemo kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Bi. Sauda alikuwa Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha na Mipango. Bi. Sauda anachukua nafasi ya Dkt. Bernard Yohana Kibesse ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Uteuzi huu unaanza tarehe 01 Juni, 2022.

  • Amemteua Mhandisi Cyprian John Luhemeja kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Mhandisi Luhemeja ni Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Uteuzi huu unaanza mara moja.