RAIS SAMIA ATOA WITO KWA JAMII KUHUDUMIA WATOTO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi kuacha kutelekeza Watoto kwa kuwa tabia hiyo inazalisha taifa lenye wananchi wasio madhubuti.
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 25 (Silver Jubilee) ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) katika ukumbi wa JNICC.
Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa wazazi na Watanzania kuiunga mkono Serikali katika kutoa huduma kwa Watoto yatima.
Rais Samia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Taasisi za kidini kutoa huduma pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii hasa kwa wananchi wanaoishi katika mazingira duni.
Kwa upande mwingine Rais Samia ameeleza kuwa Filamu ya The Royal Tour imesaidia kutoa fursa za kibiashara kwa wanawake wajasiriamali na hivyo kuwawezesha kujiinua kiuchumi.
Vile vile, Rais Samia amewataka wanawake wajasiriamali kutumia fursa hiyo kuzalisha bidhaa bora zaidi ili waweze kujiletea maendeleo na kujiinua kiuchumi.
Hali kadhalika, Rais Samia ametoa wito kwa EOTF kuendelea kuwajengea wanawake uwezo wa elimu ya biashara kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili waweze kuuza bidhaa nje ya nchi.