Daily Archives: July 7, 2022
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS SAMIA AFUNGUA JENGO LA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO CCBRT
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika kutoa huduma za dharura na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa akina mama na watoto wachanga.
Rais Samia amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT lililogharimu jumla ya shilingi Bilioni 101 ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na vifaa vingine vya hospitali.
Aidha, Rais Samia amesema lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kumpatia mwanamke huduma bora ya uzazi tangu ujauzito, kujifungua na baadae uangalizi kwa mzazi na mtoto mchanga.
Rais Samia pia amesema uwepo wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2021/2022 – 2025/2026 wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 321 kwa kila vizazi 100,000 hadi kufikia vifo 220.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa Madaktari Bingwa wanapatikana katika Hospitali za Wilaya ili watoe huduma hii muhimu.
Hospitali hiyo ina uwezo wa kuhudumia wanawake 300 kwa siku, ikiwa na jumla ya vitanda 140 na vyumba 8 vya kujifungulia na itaweza kufanya uchunguzi wa mapema wa matibabu ya watoto waliozaliwa na ulemavu.