Daily Archives: July 20, 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ALITAKA JESHI LA POLISI KUFANYA KAZI KWA UFANISI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati na Sekretarieti zitakazoshauri namna ya kuleta mabadiliko ya utendaji kazi  wenye matokeo bora katika vyombo vya utendaji haki. 

Rais Samia amesema hayo katika hafla ya uapisho wa Viongozi mbalimbali iliyofanyika Ikulu Chamwino, akieleza kuwa Kamati hiyo itaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman. 

Aidha, Rais Samia amesema Kamati hiyo itaanza kulifanyia kazi Jeshi la Polisi na baadae katika majeshi mengine ya ulinzi na vyombo vya utendaji haki.

Rais Samia pia amesema Serikali itapitia na kurekebisha miundo, mifumo ya ajira na mafunzo, mifumo ya upandishaji vyeo, madaraka na taaluma za kijeshi.

Masuala mengine ni kutoa mafunzo kwa majeshi ya ulinzi kuhusu matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mahusiano ya Jeshi la Polisi na Taasisi zingine ikiwemo Kanuni na Sheria zinazoongoza Taasisi hizo.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa ufanisi, na kuimarisha usalama wa raia na mali zao na kuzingatia haki za binadamu