Monthly Archives: August 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AAGIZA UPELELEZI UFANYIKE KABLA YA KUWEKWA MAHABUSU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Ramadhan Kingai kuhakikisha unafanyika upelelezi na kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumuweka mtuhumiwa mahabusu.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa/Vikosi katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyoko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Aidha, Rais Samia amesema kesi za watuhumiwa 1,840 zimefutwa na kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi ambapo kuwakamata watuhumiwa hao kumeipa gharama Serikali na familia za watuhumiwa.

Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kukabiliana na changamoto za kiutawala na kiufundi, kuangalia upya mitaala ya mafunzo pamoja na kufanya mageuzi makubwa ya kimuundo na kimfumo inayoendana na mabadiliko ili kukabiliana na changamoto za sasa.

Rais Samia amesema upungufu wa mafunzo unachangia mmomonyoko wa maadili ndani ya Jeshi la Polisi hivyo Serikali imetenga shilingi bilioni 11 kwa ajili ya mafunzo ya askari polisi.

Vile vile Rais Samia amesema Serikali itaendelea kufanya uwezeshaji wa kifedha ili Jeshi hilo lifanye marekebisho ya kiutendaji katika mafunzo ya TEHAMA kuanzia ngazi za wilaya hadi mkoa.

Rais Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuacha matumizi mabaya ya fedha hususan zile za bajeti zinazopelekwa kwao na kutaka kuwa na uhusiano mzuri kati yake na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa upande mwingine, amelitaka Jeshi hilo kudhibiti matumizi ya fedha za Mifuko ya ndani ya askari polisi, fedha zitokanazo na tozo na faini pamoja na zile za Mikataba mbalimbali inayosainiwa na Jeshi hilo.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan afungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi-Moshi Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kilichofanyika katika Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika hule ya Polisi Tanzania (TPS)Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye hule ya Polisi Tanzania (TPS) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu (IGP) Omari Mahita mara baada ya kufungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kilichofanyika katika hule ya Polisi Tanzania (TPS) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura pamoja na Makamanda wengine wa Jeshi hilo mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye hule ya Polisi Tanzania (TPS) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.