RAIS SAMIA AZINDUA TUME YA KUANGALIA JINSI YA KUIMARISHA TAASISI ZA HAKI JINAI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Taasisi za Haki Jinai kuendesha na kusimamia haki jinai kwa kuzingatia misingi ya sheria, weledi, usawa, uadilifu pamoja na mila na desturi zetu.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akizundua Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Chamwino.
Aidha, Rais Samia amesema Tume hiyo imeundwa kutokana na kuvurugika kwa mifumo ya haki jinai ambayo inachangiwa na kupuuzwa kwa mifumo ya maadili na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi wasio na uwezo kupoteza haki zao.
Taasisi zitakazofanyiwa tathmini na Tume hiyo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Rais Samia pia ameiagiza Tume hiyo kupitia na kuangalia mifumo ya utendaji ya Taasisi hizo na kufanya mabadiliko ya mafunzo, mifumo ya ajira, matumizi ya TEHAMA pamoja na fikra za kiutendaji na mahusiano kati ya taasisi hizo na raia.
Vile vile, Rais Samia amezitaka taasisi hizo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa.
Tume hiyo yenye Wajumbe 12 itaanza kufanya kazi kuanzia tarehe 01 Februari hadi tarehe 31 Mei, 2023.