Daily Archives: May 8, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ASHIRIKI MKUTANO WA DHARURA SADC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhuria Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkutano huo wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervention Brigade (FIB) umefanyika leo mjiniWindhoek nchini Namibia.

Aidha, mkutano huo umetoa tena wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.

Mkutano huo pia umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2023.

Vile vile mkutano huo umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi  wa Kongo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la SADC kutoka katika Kikosi cha Kudumu cha Jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama.  

Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Namibia Mhe. Dkt. Hage Geingo; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Rais wa DRC Mhe. Félix Antoine Tshisekedi;  Waziri wa Mahusiano ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola Mhe. Balozi Téte António; Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Harry Mkandawire; pamoja na  Balozi wa Zambia nchini Namibia Mhe. Stephen Katuka.