Daily Archives: July 4, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA YA MSAADA WA MAENDELEO INAYOFADHILIWA NA EU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa Mikataba 3 ya msaada wa maendeleo inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) wenye thamani ya Euro milioni 179.35 sawa na Shilingi bilioni 455.09 za Kitanzania.  

Aidha, Rais Samia ameshuhudia kutangazwa kwa fedha za msaada wa bajeti ya Serikali zilizotolewa na EU kiasi cha Euro milioni 46.11 sawa na Shilingi bilioni 117.036 za Kitanzania kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023.

Fedha hizo zitaelekezwa katika sekta za maendeleo hasa katika uchumi wa Buluu, uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na uimarishaji mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha serikalini.

Katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Hazina Rais Samia ameishukuru EU kwa kuwa msaada huo ni matokeo ya ziara aliyoifanya Brussels, Ubelgiji alipokutana na Rais wa Tume ya Ulaya Mhe. Ursula Von der Leyen.

Msaada huo uliotolewa kwa Serikali unaendana na mipango mkakati ya kisekta na maendeleo nchini, hususan Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.

Aidha, Rais Samia amesema Programu hizo pia zitaendana na kaulimbiu ya Mwaka wa Fedha wa 2023/24, kama ilivyopitishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC): “Kuongeza kasi ya kufufua uchumi, kukabiliana na kupunguza mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha sekta zenye tija kwa maisha bora“.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Akutana na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Ikulu Mkoani Chamwino tarehe 04 Julai, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa Nchini Mhe. Manfredo Fantl, wakati Balozi Fantl alipofika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma 04 Julai, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa Nchini Mhe. Manfredo Fantl, wakati Balozi Fantl alipofika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma 04 Julai, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa Nchini Mhe. Manfredo Fantl, mara baada ya mazungumzo yao Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma 04 Julai, 2023.