Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika ni pamoja na janga la rushwa ambalo linadhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango na mikakati ya kujikomboa kiuchumi.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika na maadhimisho ya utekelezaji wa miaka 20 ya Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa yaliyofanyika AICC.
Aidha, Rais Samia amesema viongozi wote barani Afrika hawana budi kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa.
Vile vile, Rais Samia amewataka viongozi kutafakari na kuchambua kwa dhati masuala ya rushwa ili kubainisha changamoto au vikwazo vya mapambano hayo na kuchukua hatua muafaka.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kibajeti na kimfumo ikiwemo kuanzisha taasisi zinazosimamia utawala bora na haki za binadamu nchini.
Rais Samia pia amesema Serikali imewekeza zaidi katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayosaidia kupunguza mawasiliano ya ana kwa ana katika kutoa huduma kama michakato ya zabuni, usajili wa biashara na namba ya mlipa kodi ili kupunguza mianya ya rushwa.
Kupitia Divisheni ya Mahakama Kuu inayosikiliza kesi za washtakiwa wa makosa ya rushwa kubwa, Serikali imeokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya Shilingi bilioni 139 kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2021/22.