Daily Archives: July 18, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mhe. Jecha Salim Jecha.

Kifo cha marehemu Jecha kimetokea tarehe 18 Julai, 2023 katika hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Rais Samia amepokea taarifa za kifo cha marehemu Jecha kwa majonzi na masikitiko makubwa.  

Vile vile, Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa kufuatia kifo cha Bernard William Mkapa (Mwenye Mkuti) ambae alikuwa kaka yake.

Rais Samia amewaomba wanafamilia wote wawe na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na amewaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi, Amina.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AKUTANA NA RAIS NOVÁK WA HUNGARY

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kuendeleza majadiliano ya kidiplomasia, Tanzania na Hungary wamebainisha maeneo mapya ya ushirikiano.

Maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na biashara na uwekezaji, elimu, utalii na pia uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake.

Rais Samia amesema hayo leo akiwa na mgeni wake Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novák aliyepo Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku 3 wakati wakizungumza na vyombo vya habari.

Wakati huo huo, Rais Samia ametoa wito kwa raia wa Hungary kuja kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini Tanzania.

Rais Samia amesema idadi kubwa zaidi ya watalii wapatao 7,188 kutoka Hungary wametembelea Tanzania kwa mwaka 2022 na anatarajia kuwa baada ya ziara ya Rais Novák idadi hiyo itaongezeka.

Kwa upande wake Rais Novák ametoa mwaliko kwa Rais Samia kushiriki katika mkutano wa masuala ya idadi ya watu utakaofanyika mwezi Septemba na mkutano wa viongozi wanawake utakaofanyika mwakani nchini Hungary.

Hungary na Tanzania zimetia saini Hati ya Makubaliano kuhusu ushirikiano wa ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) utakaotolewa baina ya nchi hizo mbili.