Daily Archives: August 10, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TEKNOLOJIA YA 5G ITARAHISISHA UTOAJI WA HUDUMA – SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inasomana na taasisi zinazosimamia sera hizo.

Rais Samia ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa 2Afrika na matumizi ya teknolojia ya 5G iliyofanyika katika ofisi za kampuni ya Airtel zilizopo Tanki Bovu.

Aidha, Rais Samia amesema misingi imara kwenye TEHAMA na mifumo ya mawasiliano kisera, kisheria na kitaasisi itawezesha kujenga uchumi jumuishi wa kidijitali (Digital Inclusive Economy) na kuinua maisha ya wananchi mijini na vijijini.

Vile vile, Rais Samia amesema uzinduzi wa teknolojia ya 5G itarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali, ikiwemo utunzaji taarifa muhimu, ukusanyaji maduhuli ya serikali, kutuma na kupokea fedha pamoja na biashara za mitandaoni.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema kuongezeka kwa mkongo huu kutatoa fursa kwa mitandao ya simu na watoa huduma wengine kuchagua mkongo wanaotaka kutumia, hivyo kuongeza ubora na kushusha gharama za intaneti.

Mkongo wa 2Afrika unaunganisha bara la Asia, Ulaya na Afrika kwa urefu wa kilometa 45,000 na kutumiwa na zaidi ya watu bilioni 3 duniani.

Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa minara mipya 758 kwa ajili ya kupanua wigo wa mawasiliano (coverage) itakayowanufaisha Watanzania zaidi ya milioni 8 kote nchini na kupunguza gharama za kuweka mkongo kwenye hifadhi za barabara.