Daily Archives: August 19, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SERIKALI KUFANYA MABADILIKO KATIKA MASHIRIKA YA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ameridhia mapendekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji ya kufuta na kuunganisha baadhi ya taasisi na mashirika ya umma.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi za umma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa AICC.

Aidha, Rais Samia ameiagiza ofisi hiyo kushirikiana na wizara za kisekta kuanza mchakato wa kisera na kisheria kukamilisha mabadiliko hayo.

Vile vile, Rais Samia amesema mabadiliko hayo yanatokana na kuingiliana na kushabihiana kwa majukumu ya baadhi ya taasisi hivyo mpango wa kuziunganisha zitaipunguzia serikali gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi na tija kiutendaji.

Rais Samia pia ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha mpango huo unafuata utaratibu na ushirikishwaji wa wadau wanaohusika, kulinda ajira na stahiki za watumishi pamoja na mali za umma kipindi chote cha mpito.

Rais Samia ameyataka mashirika ya umma kuvuka mipaka na kuwekeza nchi jirani ili faida itakayopatikana itumike kuendesha mashirika hayo hapa nchini.

Kwa upande mwingine Rais Samia amesema serikali inatarajia kuanza mchakato wa kutunga sheria itakayobadilisha hadhi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma.