RAIS SAMIA AENDELEA NA ZIARA YA KIKAZI MKOANI MTWARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi katika ngazi zote kuwasikiliza wananchi na kujielekeza kwenye kutatua kero zao.
Rais Samia ametoa tamko hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Newala katika uwanja wa Sabasaba mara baada ya kupokea taarifa za miradi ya maendeleo wilayani humo.
Akihutubia wananchi katika uwanja wa Majaliwa wilayani Tandahimba, Rais Samia amewaagiza Madiwani kusimamia vyema fedha za Halmashauri pamoja na fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali ili waweze kuwahudumia wananchi.
Vile vile, Rais Samia ametaka viongozi wasimamie vizuri fedha za ruzuku zinazotolewa kwa wakulima ili ziweze kuzalisha zaidi.
Rais Samia pia amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha wanasimamia wakulima kupata pembejeo zinazotolewa na serikali ili kuepuka utolewaji wa takwimu za uongo na kuwanyima wakulima pembejeo hizo.
Rais Samia ameendelea na ziara yake mkoani Mtwara ambapo ameweka Jiwe la msingi jengo la utawala katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.
Hali kadhalika, Rais Samia amezungumza na wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wilaya ya Mtwara Vijijini pamoja na kusalimia wananchi wa kata ya Nanyamba.