RAIS SAMIA ASISITIZA MATUMIZI YA TEHAMA KWA JESHI LA POLISI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki (TEHAMA) kama mkakati wa kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi iliyofanyika katika bwalo la maafisa wa polisi Oysterbay.
Aidha, Rais Samia amelitaka jeshi hilo kuendelea kujipanga kupokea miradi mikubwa ya kimkakati ya TEHAMA ikiwemo mradi wa miji salama pamoja na mradi wa mfumo wa utambuzi na uchakataji wa taarifa za wahalifu.
Rais Samia pia amebainisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha mradi mwingine wa ukaguzi wa magari wa lazima wenye lengo la kuongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia wananchi, kudhibiti uhalifu na ajali za barabarani.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mpango mkakati wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai, ambayo ni pamoja na kuharakisha upelelezi wa kesi za jinai ili kuepuka mrundikano.
Vile vile, Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linachukua haraka hatua za kisheria dhidi ya mtu au kikundi chochote kinachovunja sheria za nchi.
Hali kadhalika, Rais Samia amesisitiza uimarishwaji na ushirikishwaji wa jamii kupitia polisi jamii pamoja na kutoa elimu ya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.