RAIS SAMIA APOKEA RIPOTI YA UTAFITI WA AFYA YA UZAZI NA MTOTO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha hospitali zote nchini zinakuwa na wodi maalum za watoto wachanga.
Aidha, Rais Samia amewataka kuhakikisha wodi hizo zinakuwa na watumishi wenye ujuzi, vifaa tiba na dawa muhimu kwa watoto hao wachanga.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria (2022) na ugawaji wa magari ya kubebea wagonjwa na vifaa tiba katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Rais Samia pia amezitaka Wizara ya Afya, TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kushirikiana kubeba ajenda ya kupambana na udumavu wa watoto chini ya miaka 5 na kuiwekea mpango wa utekelezaji.
Vile vile Rais Samia amezitaka Wizara hizo kupanua wigo wa uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya lishe ili kupunguza zaidi kiwango cha udumavu nchini ambacho kimepungua kutoka 34% mwaka 2015/16 hadi 30% mwaka 2022.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema matokeo chanya yaliyobainishwa na utafiti huu yanadhihirisha matokeo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali kwenye sekta ya afya.
Rais Samia amegawa seti 123 za vifaa vya huduma kwa watoto wachanga na wenye uzito pungufu, mashine 125 za mionzi, mashine 140 za kutibu dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi ambavyo vitasambazwa kwenye hospitali za Halmashauri na vituo mbalimbali vya afya nchi nzima.