Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshiriki uzinduzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Mboga na Matunda (Doha International Horticulture Expo 2023).
Maonesho haya yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujifunza na kuwekeza katika kilimo hususan kwenye teknolojia rafiki ya mazingira.
Maonesho haya yanafanyika wakati dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa chakula.
Ili kupambana na hali hii uwekezaji wa mitaji kwenye sekta ya kilimo hasa sekta hiyo ndogo ya mboga na matunda imeonekana kuwa na umuhimu ili kuongeza usalama wa chakula duniani na kutunza mazingira kwa wakati mmoja.
Serikali ya Tanzania kupitia taasisi zake mbalimbali na sekta binafsi itashiriki katika maonesho haya kwa lengo la kutafuta masoko ya mazao ya kilimo.
Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo zimekuwa zikijitosheleza kwa chakula na sasa imeweka msukumo mkubwa kwenye uwekezaji wa kilimo hasa eneo la upatikanaji wa mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji, utafiti pamoja na upatikanaji wa mbolea nafuu na viuatilifu.
Juhudi hizi zinalenga kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima na kuongeza tija na uzalishaji kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada kuuza nchi nyingine.
Sekta ya mboga na matunda ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi kwa mwaka kati ya 7% hadi 11% na kutoa fursa za ajira kwa takriban watu milioni 6.5 hasa kwa vijana na wanawake.