Author Archives: Ikulu Ikulu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani 7, amemuongezea muda Jaji wa Mahakama ya Rufani 1 na ameteua Majaji wa Mahakama Kuu 21.
Majaji wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa ni;
Mhe. Patricia Saleh Fikirini ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi – Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu ya Tanzania (Dar es Salaam).
Mhe. Penterine M. Kente ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Iringa).
Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto Mkoani Tanga.
Mhe. Lucia Gamuya Kairo ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Bukoba).
Mhe. Lilian Leonard Mashaka ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi – Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mahakama Kuu ya Tanzania (Dar es Salaam).
Mhe. Issa John Maige ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi – Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu ya Tanzania (Dar es Salaam).
Mhe. Abraham Mwampashi ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Uteuzi wa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Patricia Saleh Fikirini umeanza tarehe 05 Mei, 2021, wakati uteuzi wa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wengine umeanza leo tarehe 11 Mei, 2021.
Aidha, Mhe. Rais Samia amemuongeza muda wa miaka 2 Mhe. Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi wa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia tarehe 15 Februari, 2021.
Majaji wa Mahakama Kuu walioteuliwa ni;
Mhe. Katarina Tengia Revocati ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.
Mhe. Biswalo Eutropius Mganga ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mhe. Zahra Abdallah Maruma ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili, Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama (JDU) katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Mhe. Devotha C. Kamuzora ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Baraza la Rufani la Kodi (TRAT), Dar es Salaam.
Mhe. Chaba Messe John ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi, Masjala Kuu ya Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Mhe. Lilian Jonas Itemba ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Mhe. Awamu Ahmada Mbagwa ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofisi ya Mashtaka Dodoma.
Mhe. Ayoub Yusuf Mwenda ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka.
Mhe. Nyigulile Robert Mwaseba ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Dar es Salaam).
Mhe. John Francis Nkwabi ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu (Arusha).
Mhe. Safina Henry Simfukwe ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi.
Mhe. David Patrick Nguyale ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mhe. Frank Habibu Mahimbali ambaye kabla uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza.
Mhe. James Karayemaha ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Mhe. Emmanuel Loitare Ngigwana ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Msajili Baraza la Kodi.
Mhe. Abdi Kagomba ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Meneja wa Huduma za Sheria wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Mhe. Arafa Mpinga Msafiri ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Ikulu.
Mhe. Dkt. Ubena John ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri na Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Mzumbe.
Mhe. Dkt. Eliamini Isaya Laltaika ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini.
Mhe. Dkt. Theodora Mwenegoha ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mhe. Mwanabaraka Saleh Mnyukwa ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama.
Uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu umeanza leo tarehe 11 Mei, 2021.
Tarehe ya kuapishwa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu walioteuliwa katika uteuzi huu itatangazwa baadaye.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 03 Mei, 2021 amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bi. Kristalina Georgieva kuhusu ushirikiano kati Tanzania na IMF katika masuala ya kiuchumi.
Mhe. Rais Samia aliyekuwa ofisini kwake (Ikulu Chamwino) Mkoani Dodoma amemshukuru Bi. Kristalina aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa nchini Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.
Amemueleza juu ya hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambapo ukuaji wake umeshuka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka jana hadi asilimia 4.7 hivi sasa kutokana na changamoto za janga la Korona (Covid-19) ambalo limeathiri sekta za uzalishaji na huduma za kijamii zikiwemo utalii, afya na kilimo.
Mhe. Rais Samia amesema japo kuwa hali ya uchumi wa Tanzania bado ni nzuri, Serikali inahitaji kushirikiana zaidi na IMF kunusuru sekta zilizoathirika na janga la Korona na kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo utekelezaji wake unaendelea ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115, ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) na ujenzi wa barabara na madaraja.
Amesema pamoja na kukabiliwa na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara kama vile kuondoa dosari za kikodi na ardhi, kuimarisha utawala bora na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya nchi.
Kwa upande wake Bi. Kristalina amempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.
Bi. Kristalina amesema IMF ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la Korona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.
Ameongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola za Marekani Bilioni 650 kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya Korona.
Kufuatia ahadi hiyo, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambao wamehudhuria katika mazungumzo hayo kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.