Category Archives: Hotuba

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, WAKATI WA KUFUNGUA RASMI BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DODOMA, 13 NOVEMBA 2020

Mheshimiwa Spika;

Mara ya mwisho nilipoingia kwenye Ukumbi huu Kulifunga Bunge la 11, tulibahatika kuwa na Marais wetu Wastaafu watatu. Lakini leo, wapo wawili. Mmoja, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, ametangulia mbele za haki. Hivyo basi, kabla ya kuanza hotuba yangu, nawasihi sote tusimame tumkumbuke pamoja na wabunge wote waliofariki dunia tangu kufungwa kwa Bunge la 11. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu Mzee Mkapa pamoja na marehemu wetu wote mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika;

         Baada ya utangulizi huo, napende niseme kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza imempa dhamana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulifungua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni kwa sababu hiyo, nimekuja hapa leo kulihutubia Bunge hili kwa lengo la kutimiza masharti hayo ya Kikatiba.

Napenda nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia neema ya uhai na kutuwezesha kuiona siku ya leo. Aidha, nakupongeza wewe, Mheshimiwa Job Ndugai, Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuchaguliwa, kwa mara nyingine, kuliongoza Bunge hili ukiwa Spika. Hongera sana. Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa Naibu Spika; tena mara hii akiwa Mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Mbeya Mjini. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Tulia. Huu ni uthibitisho kwamba, nchi yetu, kupitia Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, inawaamini sana wanawake.

Kama mnavyofahamu, Makamu wetu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, naye ni mwanamama. Aidha, Bunge hili la 12 nalo lina Wabunge wengi wanawake. Kwa msingi huo, napenda nitumie fursa hii kuahidi kuwa, Serikali ninayoingoza, itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Wanawake na akinamama Oyee!!!

Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu kuwa Wabunge wa Bunge hili la 12. Mmechaguliwa kwa vile wananchi wana imani kuwa mna uwezo wa kuwawakilisha vizuri. Hivyo basi, nawasihi msiwaangushe wananchi waliowachagua. Watanzania wana imani kubwa sana na Bunge hili.

Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuridhia na kumpitisha Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ahsanteni sana.

 

Mheshimiwa Spika;

Nimekuja kulizindua Bunge hili baada ya nchi yetu kufanikiwa kumaliza Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 kwa uwazi amani na utulivu mkubwa. Kwa msingi huo, napenda nirudie kuipongeza Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia vizuri zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu; kuanzia kwenye uandikishaji wapiga kura; uchukuaji na urejeshaji fomu za wagombea; usimamizi wa kampeni na pia zoezi la kupiga kura na utoaji matokeo mapema. Kwa hakika, Tume imedhihirisha uwezo mkubwa katika kusimamia Uchaguzi bila kutegemea misaada kutoka nje. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage; Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid; Makamishna wa Tume; Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera pamoja na Watendaji wote wa Tume; hongereni sana kwa kazi nzuri.

Lakini, kwa namna ya pekee, nawapongeza kwa namna mlivyotumia vizuri fedha mlizotengewa. Kama inavyofahamika, Uchaguzi wa Mwaka huu uligharamiwa na Serikali kwa asilimia 100, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 331 kilitengwa. Hata hivyo, mpaka Uchaguzi umekamilika, Tume imetumia shilingi bilioni 262 tu. Hii ni ishara ya uadilifu mkubwa walionao Viongozi na Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hongereni sana. Natoa rai kwa Taasisi nyingine kuiga mfano mzuri wa Tume hii.

Kwa moyo wa dhati kabisa, narudia kuwashukuru Viongozi wetu wa Dini kwa kutuongoza vyema kwa sala na dua katika kipindi chote cha Uchaguzi; na hatimaye tumeweza kumaliza Uchaguzi wetu salama. Nawasihi endeleeni kuliombea Taifa letu ili libaki katika mikono ya Mwenyezi Mungu.

Narudia pia kuvishukuru vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kusimamia vizuri amani na utulivu wa nchi yetu na mipaka yake wakati wote wa Uchaguzi. Hii ni ishara kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ni imara na vinafanya kazi kwa ueledi mkubwa. Hongera sana kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Kwa namna ya pekee kabisa, natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu wote kwa kushiriki vizuri na kuonesha utulivu mkubwa kwenye Uchaguzi uliopita; kuanzia kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura, wakati wa kampeni, upigaji kura na kupokea matokeo. Hakuna shaka, Uchaguzi wa Mwaka huu, kwa mara nyingine, umeuthibitishia ulimwengu kuwa sisi Watanzania ni wapenda amani, tunajitambua, hatudanganyiki na tumekomaa kidemokrasia. Ahsanteni sana Watanzania wenzangu.

 

Mheshimiwa Spika;

Masuala yote muhimu tuliyopanga kutekeleza kwenye miaka mitano ijayo, tumeyaweka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 ambayo ina kurasa 303.  Kwa bahati nzuri, Waheshimiwa Wabunge wengi wa Bunge hili wanaifahamu vizuri Ilani hiyo kwa vile wameitumia katika kuomba kura kwa wananchi kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika.

Lakini, sambamba na masuala hayo yaliyomo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi wa mwaka 2020 – 2025, tutaendelea pia kutekeleza na kusimamia mambo yote niliyoeleza wakati nikizindua Bunge la 11, tarehe 20 Novemba, 2015.

Kama mtakavyokumbuka, kwenye Hotuba hiyo ya kuzindua Bunge la 11 nilieleza mambo mengi sana, ambayo, kimsingi, yalitoa falsafa, dira na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Baadhi tumeyatekeleza vizuri; yapo ambayo hatujayatekeleza kwa ukamilifu na mengine yapo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa hiyo, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kusimamia na kutekeleza mambo yote niliyoyaeleza kwenye Hotuba ya Kuzindua Bunge la 11. Hii ndiyo sababu nimeamua kuigawa tena Hotuba yangu ya Uzinduzi wa Bunge la 11 kwenu Waheshimiwa Wabunge ili mkaisome na hatimaye ikawaongoze katika kutekeleza majukumu yenu vizuri.

Hata hivyo, pamoja na hayo yote, naomba Mheshimiwa Spika uniruhusu nitaje baadhi ya mambo muhimu tutakayoyapa kipaumbele kikubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika;

Jambo la kwanza na muhimu tutakalolipa kipaumbele kikubwa kwenye miaka mitano ijayo ni kuendelea kulinda na kudumisha tunu za Taifa letu, yaani Amani, Umoja na Mshikamano, Uhuru wa Nchi yetu, Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Na katika hilo, naahidi kushirikiana kwa karibu sana na Rais mpya wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi. Kamwe, hatutakuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu; mwenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wetu; na pia mwenye kutaka kutishia Uhuru wetu, Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Napenda pia kutumia fursa hii kumwahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwamba, kwenye miaka mitano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Zanzibar. Kwa kifupi, naweza kusema, tutafanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuleta maendeleo kwa pande zetu zote mbili za Muungano. Na katika hilo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa hotuba nzuri aliyoitoa wakati wa kuzindua Baraza la Wawakilishi. Kwenye hotuba yake alitoa dira, mwelekeo na kutaja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi kwa hotuba nzuri. Kupitia Bunge hili, napenda nimwahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuwa, nitampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza yote aliyoahidi wakati wa Uzinduzi Rasmi wa Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Spika;

Sambamba na kulinda na kudumisha tunu za nchi yetu, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha utawala bora, hususan kwa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma pamoja na kuzidisha mapambana dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma. Kwenye miaka mitano iliyopita, tuliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha nchi yetu kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International; na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa Utafiti Jukwaa la Dunia (World Economic Forum) wa mwaka 2019.

Hata hivyo, watumishi wazembe bado wapo; wala rushwa bado wapo; na pia wezi na wabadhirifu wa mali ya umma bado wapo. Kwa hiyo, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kushughulikia matatizo hayo. Na kwa kifupi, niseme, utumbuaji majipu utaendelea. Hata hivyo, kwa upande mwingine, tutaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania. Kwa hiyo, watumishi wasiwe na wasiwasi.

 

Mheshimiwa Spika;

Kwenye miaka mitano ijayo pia, tumejipanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi. Kama unavyofahamu, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tulijitahidi kusimamia vizuri uchumi wetu, ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka. Aidha, Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka 2019; tulidhibiti mfumuko wa bei, kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 4.4 na kuongeza akiba ya fedha ya kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.2 mwezi Julai, 2020 ambazo zinatuwezesha kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.

 

Zaidi ya hapo, kwenye miaka mitano iliyopita, tuliongeza mauzo yetu ya nje kutoka Dola za Marekani bilioni 8.9 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 9.7 mwaka 2019; na pia kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.6, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 30. Aidha, tulifanikiwa kupunguza umasikini wa kipato hadi kufikia asilimia 26.4 kwa takwimu za mwaka 2017/2018. Mafanikio haya, bila shaka, ndiyo yamewezesha, mwezi Julai 2020, nchi yetu kutangazwa kuingia kundi la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi masikini. Na mafanikio hayo yamepatikana miaka mitano kabla ya muda uliopangwa, yaani mwaka 2025.

Kwa hiyo, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuendeleza mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana na tutahakikisha ukuaji uchumi unawanufaisha wananchi, hususan kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umasikini na tatizo la ajira. Na katika hilo, tunalenga kukuza uchumi wetu kwa wastani wa angalau asilimia 8 kwa mwaka na pia kutengeneza ajira mpya zipatazo milioni 8. Tutaendelea pia kuboresha sera zetu za uchumi jumla na sera za fedha (yaani macroeconomic and monetary policies), na pia kuhakikisha viashiria vyote vya uchumi; ikiwemo thamani ya sarafu yetu, mfumko wa bei pamoja na viwango vya riba; vinabaki kwenye hali ya utulivu.

Tutaongeza pia jitihada za kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba ama yenye riba nafuu, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri zetu; na pia kupitia Mifuko na Programu mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali, ambayo kwa idadi zipo 18. Baadhi ya Mifuko hiyo ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF); Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF); Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF); Mfuko wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF Microfinance Fund), Mfuko wa Kudhamini Mikopo ya Mauzo ya Nje; Mfuko wa Kilimo Kwanza. n.k. Tutaimarisha usimamizi wa Mifuko hii na kuhakikisha Watanzania wanaifahamu.

Najua Mifuko hii mingi ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu; hivyo basi, nakuagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu, hii ikawe kazi yako ya kwanza kuishughulikia; ikiwezekana, mwangalie uwezekano wa kuiunganisha baadhi ya mifuko ili ifanye kazi kwa tija zaidi na kupunguza gharama za uendeshaji. Nataka Mifuko hii ikiwasaidie wananchi wa kawaida, wakiwemo machinga, akina baba na mama lishe pamoja na wajasiriamali wengine wadogo.

Sambamba na kutoa mikopo, tutaendelea kutekeleza Program mbalimbali za kukuza ujuzi na maarifa, ikiwemo maarifa ya ujasiriamali, ili kuwapa ujuzi na uzoefu wananchi wetu utakaowawezesha kujiajiri ama kuajirika ndani na nje ya nchi. Tutaendelea pia kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili tuliouzindua mwezi Februari 2020, ambao utagharimu takriban shilingi trilioni 2.032. Tutahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa, ambao ni wananchi masikini.

Muhimu zaidi ni kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sekta binafsi itapewa umuhimu wa pekee sana. Tunataka mtu yeyote atakayetaka kuwekeza asisumbuliwe kwa kuwekewa vikwazo vya aina yoyote. Watanzania ni matajiri lakini baadhi yao wanasita kuwekeza hapa nchini kwa kuogopa kusumbuliwa na maswali yasiyo na msingi. Tunahitaji kuwa na Mabilionea wengi wa Kitanzania. Nataka Watanzania wote washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao.

Sambamba na kuwekeza, Watanzania wahamasishwe kuweka fedha kwenye Benki za hapa nchini ili kusaidia benki zetu kufanya biashara na kuimarisha mzunguko wa fedha na kupunguza riba kwa wakopaji. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania mnaonisikiliza, wakati wa kufanya mambo bila woga ni sasa. Kwenye miaka mitano ijayo pia tutafungua milango kwa sekta binafsi kufanya majadiliano na Serikali ili kutafuta mwafaka ya migogoro ya biashara (business disputes) iliyopo kwa faida ya pande zote mbili. Lengo letu ni kuona Tanzania inakuwa mahali pazuri pa kufanya biashara duniani. Kwenye miaka mitano iliyopita, tumefuta tozo 168, ambapo 114 zitahusu kilimo, mifugo na uvuvi na tozo nyingine 54 za biashara.

 

 

Mheshimiwa Spika;

Mbali na hatua hizo; kwa lengo la kukuza uchumi, kupambana na umasikini, na pia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, tunakusudia, kwenye miaka mitano ijayo, kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta zetu kuu za uchumi na uzalishaji, hususan kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, biashara na utalii. Sekta hizi ndizo zenye kuajiri Watanzania wengi. Kwa hiyo, ni wazi, tukifanikiwa kuzikuza, uchumi wetu utakua kwa kasi na hivyo kupunguza matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini.

Kwa msingi huo, kwenye KILIMO, tunakusudia kuongeza tija na kukifanya kilimo chetu kuwa cha kibiashara. Lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwandani na pia kupata ziada ya kuuza nje. Ili kufanikisha hayo, tutahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo, ikiwemo mbegu, mbolea, viatilifu/dawa na matrekta, vinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu. Tutaongeza pia eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 hadi hekta milioni 1.2 mwaka 2025 ili kupunguza utegemezi kwenye mvua.

Tutaimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji kwa kushirikisha taasisi za fedha, ikiwemo Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo pamoja na benki nyingine. Tutashughulikia pia tatizo la upotevu wa mazao (yaani post harvest loss), ikiwemo kwa kukamilisha ujenzi wa vihenge na maghala maeneo mbalimabli nchini ambayo yataongeza uwezo wetu wa kuhifadhi mazao kutoka tani 190,000 za sasa hadi tani 501,000. Takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka, nchi yetu inapoteza wastani wa kati ya asilimia 30 – 40 ya mavuno yake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa miundombinu ya kuhifadhi.  Zaidi ya hapo, tunakusudia kuanzisha bidhaa mbalimbali za huduma ya Bima ya Kilimo na pia kuingia makubaliano ya kibiashara na nchi walaji na wanunuzi wa mazao ili kupata soko la uhakika.

Mazao ya kimkakati tunayolenga kuyapa kipaumbele kikubwa ni pamba, korosho, chai, kahawa, tumbaku, mkonge, michikichi, cocoa, alizeti na miwa; lakini pia mazao ya chakula. Nchi yetu kila mwaka inaagiza tani 800,000 za ngano na kwa ujumla, tunatumia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kuagiza chakula kutoka nje. Hii ni aibu kwa nchi kama Tanzania. Hivyo basi, ni lazima tutafute majawabu ya suala hili. Na hii ndiyo ikawe kazi ya kwanza ya Waziri wa Kilimo nitakayemteua.

Lakini, zaidi ya hapo, tutaweka mkazo mkubwa kwenye kilimo cha mazao ya bustani (matunda, mbogamboga, maua na viungo), ambacho kinakua kwa kasi kubwa nchini. Hivi sasa nchi yetu inashika nafasi ya 20 kwa kuzalisha kwa wingi mazao hayo duniani na mauzo yetu ya nje yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019. Hii ndiyo sababu, hatuna budi kukiendeleza kilimo cha mazao hayo. Na katika hilo, napenda kuriafu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha uzafirishaji wa mazao ya bustani, lakini pia minofu ya samaki pamoja na nyama. Wakulima wetu ni lazima watajirike na shughuli wanazozifanya; hivyo basi, Mawaziri wa Kilimo, Biashara, Mambo ya Nje na Mabalozi wajipange vizuri kwa hili.

Kwa upande wa MIFUGO, kama mnavyofahamu, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa mifugo Barani Afrika. Tuna ng’ombe milioni 33.4; mbuzi milioni 21.3; kondoo milioni 5.65; punda 657,389; lakini pia tuna idadi kubwa ya kuku, bata, kanga, n.k. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, sekta hii bado haijatunufaisha vya kutosha.

Kwa kuzingatia hilo, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kuikuza sekta ya mifugo ili ichangie ukuaji uchumi na kupunguza matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini. Tutaongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta 2,788,901 za sasa hadi hekta 6,000,000. Tunataka wafugaji wasiteswe na mifugo yao. Mifugo ni utajiri. Sambamba na hayo, tutahamasisha ufugaji wa kisasa; tutaongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora na pia kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo viwandani kutoka tani 900,000 hadi milioni 8.

Zaidi ya hapo, tutakamilisha ujenzi wa machinjio saba unaoendelea maeneo mbalimbali nchini, ambapo, kwa pamoja, zitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 6700 na mbuzi 11,000 kwa siku. Ujenzi wa machinjio hizo sio tu utasaidia kupatikana kwa nyama bora itakayouzwa hadi kwenye masoko ya kimataifa bali pia utawezesha upatikanaji wa ngozi bora kwa ajili ya kutengeneza bidhaa za ngozi. Takwimu zinaonesha kuwa, takriban asilimia 90 ya ngozi inayozalishwa nchini kwa sasa haina ubora unaohitajika; na sababu mojawapo ni uchinjaji wanyama kienyeji. Kwa hiyo, machinjio yanayojengwa yatapunguza tatizo hilo.

Nitumie fursa hii, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za mifugo (nyama, ngozi, maziwa, kwato, n.k.). Na katika hilo, tunaahidi kutoa vivutio maalum kwa watakaowekeza kwenye viwanda hivyo ambavyo vitasaidia kuinua vipato vya wafugaji wetu na pia kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. Na hapa, nataka niweke bayana kuwa, watendaji watakaokwamisha ujenzi wa viwanda hivyo tutawashughulikia.

Mheshimiwa Spika;

Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na mabwawa. Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira. Hata hivyo, kwa sasa, mchango wake bado ni mdogo. Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu, ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Shughuli za Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2018; shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu zinaweza kuingizia Serikali mapato ya moja kwa moja ya takriban shilingi bilioni 352.1 kwa mwaka endapo mifumo ya usimamizi na udhibiti ingekuwa imara na samaki wangechakatwa hapa nchini. Hata hivyo, mapato yaliyokuwa yamekusanywa kwa kipindi cha miaka tisa (2009 hadi 2017) yalikuwa shilingi bilioni 29.79, sawa na shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka.  Kiwango hiki cha mapato hakikubaliki.

Hii ndiyo sababu, tunataka, kwenye miaka mitano ijayo, kuisimamia vizuri shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu ili Taifa letu linufaike na rasilimali zake, kwa kuhusisha sekta binafsi. Kwa bahati nzuri, tayari, mwaka huu (2020) tumetunga Sheria Mpya ya Kusimamia na Kuendeleza ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Aidha, tumepanga kununua Meli 8 za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika IFAD (4 upande wa Zanzibar na 4 upande wa Tanzania Bara) ili zishiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu. Kama mnavyofahamu, suala la uvuvi wa bahari kuu ni la Muungano. Tunakusudia pia kujenga Bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa ajira zipatazo 30,000; na tutaendelea kuihamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata samaki.

Sambamba na kusimamia Bahari Kuu, tutakuza shughuli za uvuvi kwenye Maziwa yetu Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) pamoja na Mito yetu mikubwa. Tutahamasisha wavuvi wetu wadogo kujiunga kwenye vikundi ili tuweze kuwapatia mitaji, ujuzi, vifaa na zana za uvuvi; na halikadhalika tutapitia upya tozo na maeneo mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia uwekezaji. Tutahamasisha pia watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa kutumia vizimba. Sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Wateule wote wa sekta hii ni lazima walisimamie hili.

Mheshimiwa Spika;

Ni ndoto kufikiria kwamba utaweza kukuza uchumi au kupambana na umasikini pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira bila kuelekeza nguvu katika kukuza sekta ya viwanda. Duniani kote, sekta ya viwanda ndiyo mhimili mkuu wa kukuza uchumi, kupambana na umasikini pamoja na matatizo ya ajira. Kwenye miaka mitano iliyopita, tulifanikiwa kujenga viwanda vipya takriban 8,477 ambavyo vilitengeneza ajira zipatazo 480,000, ambapo Mkoa wa Pwani uliongoza kwa kujenga viwanda vingi.

Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendeleza jitihada za kukuza sekta hiyo. Mkazo mkubwa tutauweka kwenye viwanda vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini (mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi); vyenye kuajiri watu wengi; na ambavyo bidhaa zake zinatumika kwa wingi hapa nchini (nguo, bidhaa za ngozi, mafuta ya kula, sukari, saruji, n.k.).

Ili kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, tutaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kuangalia masuala ya kodi na kuondoa vikwazo na urasimu. Pamekuwepo na urasimu mwingi na kusumbuliwa kwa wawekezaji kwa kuzungushwa zungushwa na hivyo kuwafanya wakate tamaa. Mimi nataka mwekezaji mwenye fedha akija apate kibali ndani ya siku 14. Kwa sababu hiyo, nimeamua suala la uwekezaji ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kulihamisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mwenyewe. Lakini, zaidi ya hapo, tumepanga kujenga Ukanda na Kongani (clusters) za viwanda kila mkoa kulingana na mazao na maliasili zinazopatikana.

 

Mheshimiwa Spika;

Kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini. Mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. Zaidi ya hapo, kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7. Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge la 11 kwa kutoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa mafanikio haya.

Nina imani kuwa Bunge hili la 12 litafuata nyayo za Bunge la 11. Na katika hili, napenda niliarifu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa madini yetu, (kama tulivyofanya kwa kujenga Ukuta Mirerani) kwa kuimarisha Sheria zetu ili madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato. Aidha, tunakusudia kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kwa kuzingatia mfano wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick yaliyowezesha kuundwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Corporation. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel, copper, n.k. Aidha, tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.

Lakini, kuhusu madini pia, kwenye miaka mitano ijayo pia tutaendelea kuliimarisha Shirika letu la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini; kuwawezesha wachimbaji wetu wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapatia mafunzo, mikopo pamoja na vifaa. Na katika natambua kuwa, wapo baadhi ya watu wamepewa leseni za utafiti na uchimbaji lakini hawajazifanyia kazi; tutazifuta leseni zao, na maeneo hayo kuyagawa kwa wachimbaji wengine, hususan wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kukuza sekta ya madini.

Tutaendelea pia kuimarisha masoko ya madini pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini. Tunataka madini yachimbwe hapa Tanzania, yachenjuliwe, yayeyushwe na kisha bidhaa za bidhaa za madini zitengenezwe hapa hapa Tanzania; na ndipo ziuzwe nje ama watu kutoka nje waje kununua bidhaa za madini hapa nchini. Ni imani yetu kuwa, kutokana na hatua tulizopanga kuzichukua sekta ya madini itaweza kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika;

Utalii ni sekta nyingine ambayo tutaipa mkazo mkubwa kwenye miaka mitano ijayo. Sekta hii imeajiri takriban watu milioni 4. Kwenye miaka mitano iliyopita, ilikua kwa kiwango cha kuridhisha, ambapo idadi ya watalii waliotembelea nchini iliongezeka kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii 1,510,151 mwaka 2019. Mapato nayo yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019. Nitumie fursa hii kuipongeza Hifadhi yetu ya Taifa ya Serengeti kwa kuchaguliwa kuwa Hifadhi Bora Barani Afrika kwa mwaka 2020.

Kwenye miaka mitano ijayo, tumejipanga kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 5 mwaka 2025 na mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 za sasa hadi Dola za Marekani bilioni 6. Hatua tutakazochukua ni pamoja na kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ikiwemo kukuza utalii wa mikutano na uwindaji wanyamapori; kuimarisha utalii wa fukwe; kujenga miundombinu ya kuwezesha meli za utalii kuzuru nchini na kuongeza kasi ya utangazaji wa vivutio vyetu. Vilevile, tutazihamaisha taasisi na watu binafsi kuanzisha ranchi, mashamba na bustani za wanyama, kama inavyofanyika nchi nyingine, ili kuzuia ujangili na kukuza utalii; lakini pia kuongeza vipato na fursa za ajira kwa Watanzania. Na katika hilo, napenda kuwaarifu Watanzania, kupitia Bunge hili Tukufu kuwa, tumepunguza bei kwa ajili ya kupata wanyama wa mbegu. Mathalan, bei ya nyati wa mbegu imepungua kutoka Dola za Marekani 1,900 hadi kufikia shilingi laki mbili; Pofu kutoka Dola za Marekani 1,700 hadi shilingi 310,000 na Swala kutoka Dola za Marekani 150 hadi shilingi 90,000. Hivyo basi, nawasihi Watanzania wenzangu, popote walipo, kuchangamkia fursa hiyo; ambayo itachochea pia uanzishaji wa butcher za wanyama pori.

Zaidi ya hapo, tutaendelea kupitia upya kodi na tozo mbalimbali ili kuzifuta ama kupunguza kodi zenye kero. Kwenye miaka mitano iliyopita, tulipunguza ada ya leseni ya biashara ya utalii kwa wakala wa kusafirisha watalii yenye idadi ya magari chini ya manne kutoka Dola za Kimarekani 2,000 hadi Dola za Marekani 500 na matokeo yake idadi ya kampuni za Kitanzania zimeongezeka kutoka 643 mwaka 2015 hadi 1,687 mwaka 2020.

 

 

Mheshimiwa Spika;

Tuna imani, hatua hizi nilizoeleza zitatuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea ya kukuza uchumi kwa angalau asilimia 8 kwa mwaka, kuinua vipato vya Watanzania, kupunguza umasikini na kutengeneza ajira mpya milioni 8. Hata hivyo, najua, ili kufikia malengo haya, tunategemea sana kupata ushirikiano kutoka sekta binafsi. Kama mnavyofahamu, sekta binafsi ndiyo injini ya kujenga uchumi wa kisasa.

Hivyo basi, narudia kuikaribisha sekta binafsi ya hapa nchini na kutoka nje kuwekeza katika sekta nilizozitaja; na ambazo sikuzitaja. Na napenda niwahakikishie watu wa sekta binafsi kuwa, Tanzania ni mahali pazuri na sahihi pa kuwekeza. Nchi yetu ina amani na utulivu; tumebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji; nchi yetu ipo kwenye eneo la kimkatati; sisi pia ni Wanachama wa jumuiya mbili, EAC na SADC, ambazo zina soko la watu takriban milioni 500. Kwa hiyo narudia, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza hapa nchini. Na kwa bahati nzuri, tangu mwaka jana, tumeanza kutetekeleza Mpango wetu wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (yaani Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment in Tanzania). Hivyo basi, mazingira ya biashara na uwekezaji, kwenye miaka mitano ijayo, yanatarajiwa kuwa bora zaidi.

 

Mheshimiwa Spika;

Ili kukuza uchumi pamoja na sekta za uzalishaji ni lazima tuimarishe miundombinu, hususan ya usafiri na nishati ya umeme. Kamwe, huwezi kukuza sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, uchimbaji madini na utalii bila kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri pamoja na upatikanaji wa huduma za umeme. Kwa hiyo, kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita, tutaendelea kuweka mkazo mkubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya usafiri na kuboresha huduma za usafirishaji. Tutakamilisha miradi tuliyoianzisha na kuanza kutekeleza miradi mipya. Na katika hilo, tumepanga, kwenye miaka mitano ijayo, kukamilisha ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na kuanza ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 6,006; ili hatimaye tuweze kufikia lengo letu la kuunganisha mikoa na wilaya zote kwa barabara za lami. Barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi na nyingine zinatokana na ahadi nilizotoa kipindi cha Kampeni. Tumepanga pia kukamilisha ujenzi wa madaraja 7 na kuanza mengine 14, likiwemo Daraja la Kigongo – Busisi, Wami na Pangani.

Zaidi ya hapo, tutaendelea kushughulia tatizo la msongamano wa magari kwenye miji na majiji yetu, hususan Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na hapa Dodoma, ambako tumepanga kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne yenye urefu kilometa 110; ambapo Wakandarasi wawili tayari wamepatikana na ujenzi utaanza hivi karibuni.

Kwa upande wa usafiri wa reli, tumepanga kuendelea kuimarisha usafiri wa Reli ya Kati na TAZARA.  Aidha, tutakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Dodoma na kuanza ujenzi wa vipande vya reli ya Mwanza – Isaka; Makutopora – Tabora; Tabora – Isaka – Tabora – Kigoma na Kaliua – Mapanda – Kalema. Zaidi ya hapo, tutanunua vichwa vya treni ya njia kuu 39 na kukarabati 31; tutanunua mabehewa ya mizigo 800 na kukarabati 690; na pia tutanunua mabehewa 37 ya abiria na kukarabati 60.

Kuhusu usafiri wa majini, tumepanga kukamilisha upanuzi wa bandari zetu kuu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na zilizopo kwenye Maziwa yetu Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa). Tumepanga pia kununua meli mpya ya mizigo kwa ajili ya kutoa huduma Bahari ya Hindi. Tutakamilisha ujenzi wa meli mpya, kukarabati meli ya Mv. Butiama na kuanza ujenzi wa meli ya kubeba mabehewa (ferry wagon) Ziwa Victoria. Tutaikarabati MV. Liemba na MT. Sangara pamoja na kuanza ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na mizigo tani 400; na nyingine kubwa ya kubeba mizigo tani 4,000 kwenye Ziwa Tanganyika.

Kuhusu usafiri wa anga, tutajenga kiwanja kipya cha Msalato, tutafanya upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege 11, vikiwemo vya Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga, Tabora, Mtwara na Songea na pia kujenga kwa kiwango cha lami njia za kutua na kuruka ndege kwenye viwanja vya Iringa, Lake Manyara, Tanga, Musoma, Lindi, Kilwa Masoko, Njombe, Singida na Simiyu. Zaidi ya hapo, tutanunua ndege mpya tano, ambapo kama nilivyosema, moja itakuwa ya mizigo.

Ujenzi wa miundombinu hii ya usafiri pamoja na uboreshaji wa huduma za usafirishaji sio tu utachochea shughuli za uchumi na uzalishaji lakini pia itakuwa ni hatua nzuri ya kuelekea kufikia malengo yetu ya kuifanya nchi yetu kuwa lango kuu la biashara kwenye Ukanda huu; na hivyo kuweza kunufaika na nafasi ya kijiografia.

 

Mheshimiwa Spika;

Kuhusu sekta ya nishati, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya nishati na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme. Na katika hilo, tunakusudia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na kuanza ujenzi wa miradi mingine ya umeme wa maji Ruhudji Megawati 358; Rumakali Megawati 222; Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa gesi asilia Mtwara Megawati 300; Somanga Fungu Megawati 330, Kinyerezi III Megawati 600 na Kinyerezi IV Megawati 300; pamoja na miradi mingine midogo midogo. Aidha, tunakusudia kuzalisha umeme Megawati 1,100 kwa kutumia nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi).

Tumepanga pia kukamilisha Miradi wa kusafirisha umeme wa Msongo wa kilovoti 400 wa Singida – Arusha – Namanga na Iringa – Mbeya – Tunduma ambayo itaunganisha nchi yetu na majirani zetu wa Kenya na Zambia. Tutatekeleza mingine ya kuunganisha maeneo ya humu nchini kwenye Gridi ya Taifa, ikiwemo Kigoma. Kwenye miaka mitano iliyopita, tulitekeleza miradi mingi ya kusafirisha umeme na hivyo kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta; na tukaweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 719 kwa mwaka.

Kuhusu umeme pia, kwenye miaka mitano ijayo, tumepanga kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikishiwa umeme, ambapo idadi yake haizidi 2,384. Kwenye miaka mitano iliyopita, kwa takwimu za hadi jana, tumefikisha umeme kwenye vijiji 9,884; kutoka vijiji 2,018 mwaka 2016. Nchi yetu ina vijiji 12,280. Miradi hii yote ya umeme itakapokamilika, sio tu itatuwezesha tuwe na umeme wa kutosha na kufikisha umeme kwenye maeneo yote nchini, bali pia itatufanya tuwe na ziada ya kuweza kuuza nje.

Sambamba na hayo, kuhusu nishati, kwenye miaka mitano ijayo, tutaanza utekelezaji wa Miradi ya kielelezo (flagship projects) ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi. Zaidi ya hapo, tutaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani, kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Mheshimiwa Spika;

Dunia hivi sasa ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (yaani The Fourth Industrial Revoulution) ambayo yanaongozwa na sekta ya mawasiliano (ICT). Shughuli nyingi duniani, kwa sasa, zinafanyika kwa kutumia TEHAMA. Hivyo basi, sisi nasi hatuna budi kwendana na kasi hiyo ya kukua kwa sekta ya mawasiliano. Kwa msingi huo, tumepanga, kwenye miaka mitano ijayo, pamoja na masuala mengine, kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu, hususan Wilayani, tutaongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (yaani broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 mwaka 2025. Aidha, tumepanga kuongeza watumiaji wa internet kutoka asilimia 43 ya sasa hadi asimilia 80 mwaka 2025 na pia kuboresha matumizi ya simu za mkononi ili kupatikana nchi nzima. Zaidi ya hapo, tutatoa kipaumbele kwenye masuala ya utafiti na ubunifu kwenye TEHAMA; tutawatambua na kuwasajili wataalam wote wa TEHAMA; na tunakusudia kuweka anuani za makazi (postikodi) maeneo mbalimbali nchini. Tutaimarisha pia usalama kwenye masuala ya Mawasiliano.

Sambamba na kukuza huduma ya mawasiliano, tunakusudia kuendelea kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Kuhusu AFYA, kama unavyofahamu, kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3). Vilevile, tumepunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka wastani wa vifo 11,000 kwa mwaka mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa 3,000 hivi sasa na halikadhalika rufaa za kupeleka wagonjwa nje zimepungua kwa asilimia 90 baada ya kuimarisha huduma za kibingwa.

Kwa msingi huo, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, hususan zahanati, vituo vya afya na Hospitali za Wilaya kwenye maeneo ambako hazipo. Tutaimarisha pia upatikanaji wa dawa, vifaa na vitendanishi na kuongeza watumishi wa afya pamoja na kuimarisha Mifuko yetu ya Bima ya Afya ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi wote kupata Bima ya Afya. Wakati wa ugonjwa wa corona, mbali na kumtunguliza mbele Mwenyezi Mungu, tiba za asili au tiba mbadala zimesaidia sana. Hivyo basi, kwenye miaka mitano, tunakusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba mbadala. Hatupaswi kudharau dawa zetu za asili ama tiba mbadala; na kwa sababu hiyo, matibabu na maduka rasmi ya dawa za asili yataruhusiwa.  Zaidi ya hapo, tutaimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi ili kufikia viwango vya kimataifa. Tunataka huduma zote za afya zipatikane hapa nchini; na ikiwezekana watu kutoka nje waje kutibiwa hapa nchini. Na kimsingi, tayari wameanza kuja kutibiwa.

Kwenye ELIMU, tutaendelea kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo; tutaongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuongeza idadi ya wanufaika. Aidha, tutaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu, ikiwemo shule, madarasa, mabweni, maabara, maktaba, ofisi na nyumba za walimu, hosteli pamoja na kumbi za mihadhara. Tutahakikisha tunaendelea kuboresha elimu inayotolewa ili iweze kutoa maarifa na ujuzi wa kutosha kwa wahitimu. Tutahimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati, hususan kwa wanafunzi wa kike; ambapo tunakusudia kujenga Shule moja ya Sekondari kwenye kila Mkoa kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana. Tutaweka pia mkazo mkubwa kwenye elimu ya ufundi. Na katika hilo, tunalenga kuanzisha vituo mahiri vya mafunzo kwa taasisi za elimu ili kuzalisha vijana wenye uwezo unaohitajika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 75 kimepangwa kutumika: Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam itabobea katika TEHAMA, Taasisi ya Teknolojia Mwanza itabobea kwenye masuala ya Ngozi, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kitakachobobea katika taaluma za usafiri wa anga na Chuo cha Ufundi Arusha kitabobea katika nishati jadidifu.

Kuhusu MAJI, mafanikio makubwa sana yamepatikana kwenye miaka mitano iliyopita. Tumetekeleza miradi ipatayo 1422 yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 2.2. Hii imefanya upatikanaji wa maji safi na salama uongezeke kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwaka 2020 kwa vijijini; na kwa mijini kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020.

Hata hivyo, napenda nikiri, nilipokuwa kwenye Kampeni moja ya changamoto kubwa niliyoelezwa na wananchi ilikuwa shida ya maji, hususan maeneo ya vijijini. Kwa msingi huo, kwenye miaka mitano ijayo, tutajitahidi kuelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia, ikiwemo kwa kuhakikisha fedha zinazopelekwa vijijini kutekeleza miradi ya maji zinatumika vizuri. Nataka kuona miradi ya maji inayojengwa inakamilika kwa wakati. Watendaji wawe wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Mito na Maziwa yetu yatumike kikamilifu katika kuwafikisha maji kwa wananchi.

Kwenye miaka mitano ijayo pia, tutaimarisha Mfuko wa Taifa wa Maji ili kuuongezea uwezo wa kifedha wa kutekeleza miradi ya maji. Tutakamilisha pia miradi mikubwa, ukiwemo wa Miji 28 utakaogharimu shilingi trilioni 1.2; Mradi wa Maji wa kutoa maji Ziwa Victoria unaogharimu takriban shilingi bilioni 600 na Mradi Mkubwa wa Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 520. Lakini, nitumie fursa hii pia kuwasihi Watanzania kulinda vyanzo vya maji na miundombinu inayojengwa. Na nitoe wito kwa viongozi wote, mkiwemo Waheshimiwa Wabunge, kulifanya suala la kutunza vyanzo vya maji na miundombinu yake kuwa ajenda muhimu katika shughuli zenu.

 

Mheshimiwa Spika;

Kwenye miaka mitano ijayo, tumejipanga kuendelea kuimarisha na kukuza uhusiano wetu na nchi mbalimbali kwa kuzingatia Sera yetu ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo diplomasia ya kiuchumi. Tutakuza urafiki na ujirani mwema na pia tutashiriki kikamilifu kwenye shughuli za Kikanda, Kibara na Kimataifa, hususan kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Tutaendelea pia kushiriki kwenye shughuli za kulinda amani.

Halikadhalika, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendeleza jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia, kulinda uhuru na haki za wananchi na vyombo vya habari. Hata hivyo, ningependa kukumbusha kuwa, lengo la demokrasia ni kuleta maendeleo na sio fujo; na hakuna demokrasia isiyo na mipaka. Aidha, Uhuru na Haki vinakwenda samabamba na wajibu. Hakuna uhuru au haki isiyo na wajibu. Vyote vinakwenda sambamba.

 

 

Mheshimiwa Spika;

Kama nilivyoahidi wakati wa kipindi cha Kampeni, kwenye miaka mitano ijayo tutaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo (machinga, mama lishe, baba lishe, waendesha boda, bajaji, n.k.). Kama mnavyofahamu, kwenye miaka mitano iliyopita, tulianzisha utaratibu wa kutoa Vitambulisho Maalum kwa wajasiriamali wetu wadogo. Kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kuviboresha vitambulisho, ikiwemo kuweka picha na taarifa nyingine muhimu, kama ilivyo kwenye Vitambulisho vya Taifa au Pasipoti. Hii itawawezesha wafanyabiashara watakaotumia vitambulisho hivyo kutambulika, ikiwemo kwenye benki na hivyo kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara. Hii itawawezesha wafanyabiashara wetu wadogo kukua na kutajirika. Na hilo ndilo lengo letu. Tunataka wafanyabiashara wetu wadogo wawe wanakua na kutajirika; na sio siku zote wabaki kuwa wafanyabiashara wadogo.

Kwenye miaka mitano ijayo pia, tutakuza sekta ya sanaa, michezo na utamaduni ambayo inakua kwa kasi kubwa hivi sasa. Kama nilivyoahidi wakati wa Kampeni, tutaikuza zaidi sekta hii, hususan kwa kuimarisha usimamizi wa masuala ya Hati Miliki ili wasaniii waweze kunufaika na kazi zao; tutahuisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu, ikiwemo kupata mafunzo na mikopo. Tutaanza pia kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuziandaa Timu zetu za Taifa. Na katika hilo, napenda kutumia fursa hii kuitakia heri Timu yetu ya Taifa, Taifa Stars, kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia baadaye leo pamoja na Mwanamasumbwi wetu, Hassan Mwakinyo, ambaye naye ana pambano letu. Watanzania tunataka ushindi.

Mheshimiwa Spika;

Kwenye miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma. Viongozi na Watumishi wote wa Serikali wenye kustahili kuhamia Dodoma tayari wamehamia. Kwenye miaka mitano ijayo, tutakamilisha ujenzi wa ofisi na pia kuendelea na ujenzi wa makazi ya watumishi. Zaidi ya hapo, tutaendelea kutekeleza miradi ya miundombinu, ambayo tayari nimeitaja (barabara ya njia nne, Uwanja wa ndege wa Msalato) na kushughulikia suala la upatikanaji maji katika Jiji la Dodoma.

Masuala mengine ambayo tutayapa kipaumbele ni kama ifuatavyo:

  • Uendelezaji na uboreshaji wa makazi wa wananchi, ambapo tutahakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa gharama nafuu na mikopo ya ujenzi inapatikana kwa riba nafuu;
  • Tutashughulikia pia masuala ya mabadiliko ya tabianchi;
  • Tutashughulikia masuala ya watu wa makundi maalum, ikiwemo wazee na watu wenye ulemavu;
  • Tutaendeleza vita dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya;
  • Tutaimarisha sekta ya misitu na nyuki, ikiwemo kwa kuanzisha viwanda vya mazao ya nyuki ili sekta hiyo itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Tutahamasisha pia ufugaji wa nyuki.
  • Tutahakikisha wamiliki wa magari wanatoa mikataba kwa madereva ili kuipa hadhi inayostahili kazi hiyo na kuchochea shughuli za huduma za usafirishaji. Na katika hiyo, ikiwezekana, itatungwa Sheria mahususi.

Tutashughulikia pia kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, n.k. Na katika hili napenda kuwaagiza viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa kuhakikisha wanatenga siku maalum za kukutana na wananchi kwenye maeneo yao ili kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

 

Mheshimiwa Spika;

Kwa ujumla, mambo tuliyopanga kutekeleza ni mengi; ni mengi sana. Baadhi nimeyaeleza na yapo mengine mengi ambayo yameelezwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM yenye kurasa 303, lakini kwa sababu ya muda sitoweza kuyaeleza yote. Hivyo basi, nawaagiza Mawaziri nitakaowateua pamoja na Watendaji kuisoma vizuri, kuielewa na kuitafsri vizuri Ilani hiyo katika Sera na Mipango Kazi ya Utekelezaji kwenye Wizara au Taasisi wanazoziongoza ili ikifika mwaka 2025, tuwe tumeitekeleza yote.

Lakini, najua, ili kuweza kutekeleza Ilani yetu vizuri, tutahitaji sana kupata ushirikiano kutoka kwenye Bunge hili. Kama mnavyofahamu, Bunge ni kiungo muhimu kati ya Serikali na Wananchi. Kwa hiyo, nina uhakika, endapo tutashirikiana vizuri, miaka mitano ijayo itakuwa ya maajabu na mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Na binafsi, sina shaka kwamba, Bunge hili litatoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali.

Hata hivyo, napenda niweke bayana kuwa, ninaposema tunaomba ushirikiano haimaanishi kwamba tunataka muunge mkono kila kitu. La hasha! Penye kukosoa kusoeni; lakini kwa hoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia. Tunahitaji constructive criticism na sio kukosoa kwa lengo la kukosoa tu. Na katika hilo, kwa upande wetu Serikali, tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bunge hili ili kuliwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo. Tutatoa pia ushirikiano kwa Mhimili wa Mahakama, ili nao uweze kutimiza majukumu yake ya kusimamia haki nchini. Kama mnavyofahamu, Mahakama ni muhimu sana katika kuongoza Serikali. Ni muhimu katika kujenga maelewano katika jamii, kudumisha amani na usalama na pia kuchochea shughuli za kiuchumi.

 

Mheshimiwa Spika;

Kwa mujibu wa Katiba yetu, mimi ni sehemu ya Bunge hili. Hivyo basi, kabla sijahitimisha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wageni wetu wote walioungana nasi kwenye tukio hili. Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!

Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”

RAIS MHE. DKT. MAGUFULI ASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI ( LAW DAY) . FEBRUARI 06, 2020

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipongezwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Job Ndugai baada ya hotuba yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Februari 6, 2020 (kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Job Ndugai pamoja na Viongozi wengine wakipiga makofi wakati kwaya ya Mahakama ikitumbuiza  kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020 

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma akizungumza mbele ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Job Ndugai akizungumza mbele ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Februari 6, 2020 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Spika Job Ndugai ,Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Agustine Mahiga , Jaji Mkuu wa Zanzibar Omary Othuman Makungu, Jaji Kiongozi Dkt. Eliezer Fereshi na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Mbarouk Salum Mbarouk  katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Februari 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Spika Job Ndugai ,Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Agustine Mahiga , Jaji Mkuu wa Zanzibar Omary Othuman Makungu, Jaji Kiongozi Dkt. Eliezer Fereshi na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Mbarouk Salum Mbarouk, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi  katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyma vya Siasa kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Februari 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, Spika Job Ndugai ,Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Agustine Mahiga , Jaji Mkuu wa Zanzibar Omary Othuman Makungu, Jaji Kiongozi Dkt. Eliezer Fereshi na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Mbarouk Salum Mbarouk  katika picha ya pamoja na Mabalozi wanao ziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Februari 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini Biswalo Mganga kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Februari 6, 2020.