Daily Archives: March 29, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA APOKEA RIPOTI YA TAKUKURU NA CAG

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi na watendaji wa Serikali kuzisoma na kuzielewa vyema taarifa za rushwa na za ukaguzi wa hesabu za Serikali ili ziwasaidie kujitathmini.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo mara baada ya kupokea taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika hafla iliyofanyika Ikulu.

Aidha, Rais Samia amesema taarifa hizo hizo zinasaidia kusimamia na kuimarisha utawala bora na kuhakikisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Serikali unafanywa kikamilifu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Bandari kufanya kazi na sekta binafsi ili kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji fedha ambapo itasaidia kudhibiti upotevu mkubwa wa fedha unaotokea bandarini.

Rais Samia pia amegiza kufanyiwa tathmini kwa Mashirika ya Umma yaliyopata hasara na kuyafuta Mashirika ambayo hayana tija kwa taifa kwa kuwa Mashirika hayo yanatumia gharama kubwa lakini hayaleti faida kwa Serikali.

Katika ripoti ya CAG jumla ya Halmashauri 14 nchini zimepata hati zenye mashaka zikiwemo Halmashauri ya Jiji la Arusha, Babati, Bahi, Geita, Kilindi, Mbinga, Musoma, Nkasi, Nyasa, Simanjiro, Songwe, Sumbawanga Manispaa pamoja na Ushetu iliyopata hati mbaya.