Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 25 Juni, 2021 amezungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kueleza kuwa Taaisisi za Dini nchini ni muhimu kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kudumisha amani, kustawisha maisha ya wananchi na kupambana na umasikini.
Mhe. Rais Samia amewasihi Watanzania kuendelea kuvumiliana kwenye tofauti za Kidini zinazojitokeza ili kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.
Amesema amani na utulivu nchini ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya taifa, hivyo ni vyema viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani kwa waumini wao.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewaomba Maaskofu na viongozi wengine wa Dini kuwakumbusha waumini wao kuhusu umuhimu wa kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Mhe. Rais Samia ametumia mkutano huo na Viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kueleza mipango ya Serikali ya miaka mitano kuwa ni pamoja na kudumisha mema yote ya Awamu zilizotangulia na kubuni mengine mapya.
Amesema Serikali imejipanga kuendeleza kukuza uchumi ili kupambana na umasikini na tatizo la ajira kwa kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amemuhaklikishia Mhe. Rais Samia kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali anayoiongoza kwa lengo la kuwaletea Wananchi maendeleo.
Askofu Mkuu Nyaisonga amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea majukumu ya Urais na kuongoza Taifa kwa utulivu na amani. Kuonyesha nia thabiti ya kushirikiana na ulimwengu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Aidha, Askofu Mkuu Nyaisonga amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutenga muda na kuwasikiliza ambapo ameelezea hatua hiyo ni kuonesha nia ya dhati katika kukuza taifa lenye mshikamano, maridhiano,na maendeleo ya kweli.