Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 16 Julai, 2021 ameanza rasmi ziara ya Kitaifa ya siku mbili Nchini Burundi kwa mwaliko wa Rais Mhe. Evariste Ndayishimiye.
Katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mechior Ndadaye Jijini Bujumbura, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais wa Burundi Mhe. Prosper Bazombanza.
Mhe. Rais Samia amefanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Rais Evariste Ndayishimiye yaliyolenga kukuza zaidi uhusiano kati ya mataifa haya mawili hususan katika kukuza biashara na uwekezaji.
Amesema biashara kati ya Tanzania na Burundi imeongezeka kutoka shilingi bilioni 83.9 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 200.1 mwaka 2019, ambapo uwekezaji kutoka Burundi ni miradi 18 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 209.42 iliyotoa ajira zipatazo 3,544 ukiwemo mradi mkubwa wa kiwanda cha mbolea kinachojengwa na kampuni ya ITRACOM wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 180.
Kwa upande wa Tanzania, Mhe. Rais Samia amesema kampuni nyingi zimewekeza Nchini Burundi zikiwemo kampuni ya Azam, Azania Group, Interpetrol, Ndaki Contractors, Tanzania Bile Acid na Benki ya CRDB.
“ hivyo basi, tumekubaliana kuendelea kushirikiana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwenye nchi zetu kwa kuondoa vikwazo vya kodi na visivyo vya kodi, ikiwemo kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Huduma za Mpakani kwenye Mpaka wetu wa Manyovu/Mugina.” amesema Rais Samia.
Vilevile, Mhe. Rais Samia na Rais Ndayishimiye wameshuhudia utiaji saini wa hati 8 za makubaliano kuhusu ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Burundi na Kifaransa nchini Tanzania, masuala ya afya, Nishati, Kubadilishana Wafungwa, Madini, Kilimo, Sekta ya Uvuvi na masuala ya Siasa na Dipolasia.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewaomba wafanyabishara wa Madini Nchini Burundi kuleta madini yao nchini Tanzania ili kuongezwa thamani katika kiwanda kinachojengwa Kahama badala ya kuuza madini hayo yakiwa ghafi pia kuuza madini yao katika masoko ya Tanzania.
Mhe. Rais Samia ametembelea Benki ya CRDB iliyopo Jijini Bunjumbura na kuzungumza na wafanyakazi wa benki hiyo ambapo amewataka kuendelea kuchapa kazi zaidi mbali na mafanikio wanayoyapata.
Pia Mhe. Rais ametembelea kiwanda cha kuzalisha Mbolea Asili cha Fertilizer Organo Mineral Industries (FOMI),na kumshukuru Mhe. Rais Ndayishimiye kwa mapokezi makubwa tangu alipoingia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mechior Ndadaye na katika maeneo mbalimbali aliyotembelea.
Mhe. Rais Samia kesho ataendelea na ziara yake nchini Burundi ambapo atakutana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini hapa na kuzungumza na Jukwaa la Wafanyabiashara wa Burundi na Tanzania.