TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 21 Agosti 2021, amemuapisha Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Mabalozi watatu wanaoiwakilisha Tanzania nje ya Nchi.

Mabalozi walioapishwa ni Mhe. Balozi Ltn. Jen. Yacoub Hassan Mohamed kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia,  Mhe. Balozi Elsie Sia Kanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Lt. Jen.Mathew Edward Mkingule kuwa Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Samia amewataka kufanya kazi kwa bidii na kuwambusha kwamba wana majukumu makubwa na wamebeba matumaini ya Watanzania.

Mhe. Rais Samia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Ole Gabriel kuhakikisha anasimamia maslahi ya watumishi wa Mahakama na kuhimiza utoaji wa haki na kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Mabalozi aliowaapisha kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine pamoja na Taasisi za Kimataifa, na amewahimiza kulinda maslahi ya Tanzania kimataifa, kutetea maslahi ya Watanzania wanaoishi nje,  kutafuta fursa za kibiashara, uwekezaji, utalii na ajira katika Taasisi za Kimataifa.

Wakati huohuo, Mhe. Rais  Samia amevitaka vyama vya siasa kuwapa nafasi wagombea Wanawake katika Uchaguzi Mkuu ujao kwasababu wana ushiriki mkubwa katika uchaguzi ikilinganishwa na wanaume.

Mhe. Rais Samia amesema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Semistocles Kaijage.

Amesema katika uchaguzi huo wagombea wa nafasi ya Urais na Makamu wa Rais walikuwa 30, kati yao wanawake walikuwa 7, katika ngazi ya ubunge wagombea walikuwa 1,257 kati yao wanawake walikuwa 293 na kwenye ngazi ya udiwani wanawake walikuwa 668 kati ya wagombea 9,231.

Pia, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wanawake kujiamini na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika siasa ili waweze kupata fursa ya kuingia katika vyombo vya maamuzi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia amevipongeza vyama vya siasa vilivyoshiriki katika hafla hiyo kwa kusema kuwa uwepo wao umethibitisha ukomavu wa kisiasa na demokrasia nchini.

Mhe. Rais ameitaka Tume ya ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulinda haki za wagombea kwa kuziangalia upya sheria zinazosimamia uchaguzi  kwa kuhakikisha kwamba Watanzania hawakosi haki ya kugombea kwa kwa makosa madogo madogo.

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia amehimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika michakato ya uchaguzi. Hii ni kwasababu shughuli nyingi duniani kwasasa ikiwemo masuala ya uchaguzi yanafanyika kwa njia hiyo ili kupunguza malalamiko ya wagombea na kuharakisha utoaji wa matokeo kwenye ngazi zote.

Hafla ya makabidhiano ya Taarifa hiyo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020,  imehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleimani Abdulla, na viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, dini na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *