TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 22 Agosti, 2021 amepokea Kombe la Ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 23 (CECAFA Challenge Cup 2021), katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amepokea Kombe hilo kutoka kwa Nahodha Msaidizi wa Timu hiyo ya Taifa ya Vijana (U23) Reliant Lusajo. Timu hiyo ya vijana ilibeba Kombe hilo baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Vijana ya Burundi kwa mikwaju ya penalti 6-5.

Mhe. Rais Samia ameipongeza timu hiyo kwa kuchukua Kombe hilo na ameeleza kuwa ana matumiani makubwa ushindi wao huo utazihamasisha timu zetu nyingine za Taifa kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Aidha, Mhe. Rais ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho na Vyama vya Michezo, vilabu pamoja na wanamichezo wenyewe, kujipanga vizuri ili kuweza kuleta matokeo mazuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Pia, Mhe. Rais ametaka kuangaliwa vyema kwa wanamichezo nchini ili pindi wanapostaafu au kuumia wawe na maisha bora tofauti na hali ilivyo sasa  ambapo wengi wao wamekuwa na maisha duni yasiyo akisi mchango wao kwa Taifa.

Vilevile, Mhe. Rais Samia ameitaka Kamati ya Olimpiki kujitathmini na kuja na mkakati utakaowezesha  kuongeza idadi ya washiriki katika mashindano mbalimbali tofauti na ilivyo sasa ambapo timu husafiri na viongozi wengi zaidi ya wachezaji.

Halikadhalika, Mhe. Rais amewataka viongozi wa vilabu, Vyama na Mashirikisho ya Michezo nchini kuzingatia masuala ya utawala bora kwa kuhakikisha wanafuata Katiba, Sheria na taratibu za taasisi zao kwa kudhibiti vitendo vya wizi, ubadhirifu, upendeleo na upangaji matokeo ambavyo vinakwamisha ukuaji na ustawi wa sekta ya michezo nchini.

Mhe. Rais ameitaka sekta binafsi kuwekeza zaidi kwenye michezo nchini kwasababu imekuwa ni biashara kubwa duniani na kuipongeza Kampuni ya Azam Media Limited kwa namna inavyojitahidi kuwekeza kwenye mchezo wa mpira wa miguu na ndondi (vitasa) nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *