TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema baada ya kukamilika kwa filamu itakayo tangaza utalii, biashara na fursa za uwekezaji nchini kupitia kipindi maarufu cha Royal Tour, dunia itafahamu kuwa madini ya Tanzanite yanachimbwa Tanzania pekee.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 05 Septemba, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa Mirerani Mkoani Manyara alipokuwa njiani kuelekea katika mgodi wa Tanzanite.

Amesema filamu hiyo itaweka wazi kwa dunia kuhusu yanapotoka  madini ya  Tanzanite, hatua ambayo itaondoa utata uliopo sasa ambapo baadhi ya mataifa yanadai kuwa ni wazalishaji wa madini hayo.Mhe. Rais Samia amewataka wafanyabiashara kuacha kuuza hovyo madini ya Tanzanite kwani kufanya hivyo kunashusha thamani   ya madini hayo.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametembelea eneo la Mlima Kilimanjaro kwa kupitia lango la Marangu, ambapo amesema pamoja na mambo mengine, filamu hiyo ina lengo la kuidhihirishia dunia kwamba Mlima Kilimanjaro upo Tanzania.

Akiwa njiani kuelekea Marangu Mhe. Rais Samia amesalimiana na wananchi wa maeneo ya Boma Ng’ombe na Himo na kuwaahidi kutekeleza ahadi walizoahidi wakati wa kampeni na kutatua changamoto zinazowakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *