TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa  kwa tozo zinazotozwa na Taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta  hapa nchini zenye thamani ya shilingi Bilioni 102 kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta ili kuwapa unafuu wananchi.

Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo  leo tarehe 05 Oktoba, 2021 wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, Mhe. January  Y. Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Utekelezaji wa maagizo hayo umeenda sambamba na marekebisho ya Kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na yatachapishwa katika Gazeti la Serikali leo tarehe 05 Oktoba, 2021.

Mhe. Rais  Samia amechukua hatua hii ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

Taasisi zinazoguswa na maelekezo ya kupunguzwa kwa tozo hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania ( tozo ya kuchakata taarifa), Shirika la Viwango Tanzania ( tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta), Wakala wa Vipimo Tanzania (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali  za Mitaa (ushuru wa huduma kwenye Halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla).  Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za Jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni endapo zipo Sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta  hapa nchini,  ili kumlinda mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na  kupanda kwa bei ya mafuta.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. January Y. Makamba, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu. L. Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara  Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Ummy A. Mwalimu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame M. Mbarawa, Naibu Waziri wa Nishati Mhe.  Stephen L. Byabato, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Eliezer M. Feleshi, Katibu Mkuu Wizara ya Niashati Mhandisi Leonard R. Masanja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhe. Kheri A. Mahimbali  na watendaji wa Taasisi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *