TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii nchini ikiwemo sekta ya afya, ili wananchi waweze kunufaika na hudma hizo.

Mhe. Rais Samia, amesema hayo tarehe 16 Oktoba, 2021 katika Sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.

Katika Maadhimisho hayo, Mhe. Rais Samia amezindua mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Rufaa ya KCM na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo maalum la kutoa huduma za tiba ya Saratani kwa mionzi litakalogharimu shilingi bilioni 4 litakapokamilika, ujenzi ambao unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Mhe. Rais Samia amesema inafurahisha kuona uongozi wa hospitali hiyo kuamua kuanzisha vitengo vipya  mbalimbali vya utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi jambo ambalo litaongeza utalii wa tiba kwa wagonjwa wa ndani na nje.

Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na hospitali mbalimbali zinazomilikiwa na Taasisi za Dini zinazotoa huduma za tiba ikiwemo Hospitali ya KCMC ili kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa.

Mhe. Rais Samia amesema kitendo cha uongozi wa hospitali hiyo kuweka mashine za kisasa ikiwemo MRI, CT Scan, kuanzisha jengo la tiba ya Moyo, Figo na Kansa na kutoa huduma za kibingwa kitapunguza rufaa ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi ambapo hivi sasa wagonjwa kutoka nje ya nchi wanakuja kupata huduma za matibabu hapa nchini na kuwezesha kufikia utalii tiba kama inavyokusudiwa.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 tayari Serikali imetoa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kuimarisha huduma za dharura na ICU kwenye Hospitali ya KCMC.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hospitali hizo zinasimamiwa na miongozo ikiwemo kupewa wataalamu pamoja na huduma zote wezeshi.

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kanisa, ambapo inalipa mishahara ya watumishi wa hospitali hiyo kwa wastani wa shilingi bilioni 10 kwa mwaka.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuanzishwa kwa huduma za kibingwa bobezi katika hospitali hiyo na kuanzisha matibabu na uchunguzi wa Saratani pamoja na ujenzi wa Wodi ya wagonjwa wa Saratani, kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amepongeza hosptali hiyo kwa kutoa huduma za vipomo vya Sukari, Macho, Usikivu, Shinikizo la Damu na maradhi ya ngozi bila malipo na kutoa elimu ya UVIKO 19 pamoja na kutoa chanjo.

Pia, ametoa wito kwa watafiti kuongeza wigo wa kuhakikisha idadi ya tafiti za magonjwa mapya na yale ya milipuko zinaisaidia Serikali kujipanga kukabiliana na majanga kwa kuandaa wataalamu pamoja na vifaa tiba vya kutibu magonjwa hayo.

Mhe. Rais Samia amemaliza ziara ya kikazi mkoani  Kilimanjaro na kuwasili mkoani Arusha ambapo akiwa njiani kuelekea mkoani Arusha amezungumza na wanachi wa maeneo ya Kikatiti, Usa River na Tengeru ambapo amewaahidi wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za jamii na kuimarisha miundombinu ya barabara.

Aidha, kesho tarehe 17 Oktoba, 2021, Mhe. Rais Samia anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Arusha ambapo pamoja na mambo mengine atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi wa mkoa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *